EPUKENI WANAOWACHOCHEA KUFANYA VURUGU WANA MASLAHI BINAFSI: WAZIRI ULEGA
Dar e Salaam, 25 Novemba, 2025
Waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah Ulega amefanya ziara katika eneo la Gongolamboto kwa lengo la kukagua na kujionea uharibifu wa miundombinu ya mradi wa BRT 3 uliosababishwa na vurugu wakati wa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambapo amewaasa wananchi kujiepusha na makundi ya watu ambao wana nia ya kuchafua amani ya nchi kwa kuhamasisha vurugu na vitendo vya kihalifu jambo ambalo limegharimu maisha na mali za watu wasio na hatia.
Ziara ya Waziri Ulega imekuja siku chache baada ya ile ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Mwigulu Nchemba iliyohusisha ukaguzi wa miundombinu na mali zilizoharibiwa wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambapo takwimu zilionyesha jumla ya vituo 20 vya mabasi ya mwendokasi vilikuwa vimeharibiwa vibaya.
“Ndugu wananchi wa Gongolamboto awali ya yote naomba niwape pole waathirika wote wa tukio hili ambalo kwetu sote limeacha mshangao mkubwa, kwa ujumla linatuma ujumbe mkubwa kwetu sote kuwa sisi ni watu wamoja, tumezoea kushirikiana pamoja kwenye shida na raha, hatujazoea kuhitilafiana na kuhasimiana kiasi hiki, chuki kwetu mwiko, sasa tujiulize nani katufikisha hapa” aliongea kwa masikitiko Waziri Ulega.
Aidha Waziri Ulega ameitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Gongolamboto kuendelea kupendana, kuheshimiana na kuaminiana jambo ambalo amesema itasaidia kurejesha hali ya amani na kuruhusu miradi ya maendeleo kuendelea kutekelezwa kwa tija ukiwemo mradi wa BRT 3 ulioathirika vibaya wakati wa machafuko.
Halikadhalika katika hotuba yake kwa wananchi hao, Waziri Ulega alitangaza kuwa serikali kupitia maelekezo ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeruhusu njia ya mabasi ya mwendokasi ambayo bado miundombinu yake inaendelea kuboreshwa kutoka Gongolamboto kuelekea katikati ya jiji ianze kutumika kupitisha magari binafsi pamoja na ya abiria ili kupungiza foleni na msongamano katika eneo hilo.