News

SERIKALI INAWAJALI TUNZENI MIRADI ITAWASAIDIA KUHARAKISHA SHUGHULI ZA MAENDELEO: MHE. ULEGA

SERIKALI INAWAJALI TUNZENI MIRADI ITAWASAIDIA KUHARAKISHA SHUGHULI ZA MAENDELEO:  MHE. ULEGA

Dar es Salaam, 25 Novemba, 2025

Waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah Ulega ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi waujenzi wa mabasi ya mwendokasi wa BRT 3 katika eneo la Buguruni na kumtaka mkandarasi anayesimamia mradi huo kuongeza kasi ili kuhakikisha unakamilika haraka iwezekanavyo uanze kuwahudumia wananchi.                                                                                                 

Akizungumza na wananchi waliofika kushuhudia utekelezaji wa mradi huo sambamba na ujio wake na wataalamu katika eneo la Buguruni jirani na daraja la reli ya SGR, Waziri Ulega amewaeleza kuwa serikali inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwaondolea adha ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa zao kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakiwasilisha maombi yao kwa Mhe Waziri Ulega, baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la daraja la reli ya SGR wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwatengenezea mazingira rafiki yatakayowawezesha kutekeleza biasahara zao kwa tija huku wakitaja ukosefu wa maeneo ya kupanga bidaa zao pamoja na maegesho ya magari yanayofika kusafirisha mbao uliosababishwa na upanuzi wa barabara kuwa ni changamoto zinazosababisha washindwe kujipatia kipato.

Akijibu kero hizo Waziri Ulega amewaagiza wataalamu kuangalia uwezekano wa kubadili mpango wa kupanda miti katika baadhi ya maeneo ya barabara hiyo na badala yake waweke mpango kazi wa kuipanua sehemu yake ili wafanyabiashara wapate eneo la maegesho sambamba na kuwawezesha kuchangia pato la taifa kupitia kodi.

Kuhusu hoja ya kuwapatia wafanyabiashara eneo la biashara jirani na uzio wa kiwanda cha Bakhresa, Mhe Waziri Abdallah Ulega amewaeleza kuwa suala hilo linahusisha Wizara mtambuka ikiwemo Wizara ya Uchukuzi na hivyo akalazimika  kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila kukutana na mamlaka hizo na kutoa majibu kwa haraka kuhusu ombi lao.