News

HATUTAMVUMILIA MKANDARASI YEYOTE ANAYECHEZEA MIRADI YETU: WAZIRI ULEGA

HATUTAMVUMILIA MKANDARASI YEYOTE ANAYECHEZEA MIRADI YETU: WAZIRI ULEGA

Dar es Salaam, 25 Novemba, 2025

Waziri wa Ujenzi Mhe Abdallah Ulega amemwagiza Mkandarasi wa Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Mwendokasi BRT 4 China Geo Engineering Corporation kuhakikisha anakamilisha kazi aliyokabidhiwa kwa asilimia mia moja vinginevyo serikali itachukua hatua kwa kukiuka mkataba.

Waziri Ulega ametoa Kauli hiyo Novemba 25, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Dar es Salaam ambapo amesisitiza kuwa serikali haiko tayari kumvumilia mkandarasi yeyote ambaye hatekelezi majukumu yake kama mkataba unavyoelekeza.

Mara baada ya kukagua mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 187 Waziri Ulega amesema kuwa haipendezi kuona wananchi wanateseka kwenye foleni wakati tayari serikali imemlipa mkandarasi mabilioni ya fedha kwa kazi ambayo haionyeshi matokeo.

"Bila shaka kila mmoja wenu aliyeko hapa ameshuhudia kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huu hapa mawasiliano, kwangu mimi hili halikubaliki, tekelezeni makubaliano yaliyomo kwenye mkataba, mmeniomba niwaongezee miezi minne mbele nawaeleza wazi siwezi kabisa, nawapatia miezi miwili tu muwe mmekamilisha na kukabidhi mradi, kinyume na hapo sina majadiliano na nyinyi'' aliwaeleza Waziri Ulega.

Halikadhalika katika mradi wa BRT 4 LOT 2 wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi ya mwendokasi eneo la Afrikana Mhe Waziri Abdallah Ulega baada ya kuukagua pia alibaini utekelezaji duni wa mradi huo hali ambayo haiendani na makubaliano yaliyomo kwenye mkataba na hivyo kulazimika kutoa maelekezo kwa wahusika.

“Ni zaidi ya mara tatu nimetembelea mradi huu na kutoa maelekezo kwa Mkandarasi huyu kampuni ya Shandong Luqiao Group Co LTD lakini ukiwapa mgongo hakuna kinachoendelea, sasa wataalamu mnaosimamia mradi huu nawaagiza nendeni mkaangalie taratibu zote za kisheria za kuvunja mkataba tujiridhishe, endapo ataendelea na mtindo huu akidhani miradi yetu anaweza kuichezea anavyotaka tuvunje mkataba tutafute mkandarasi mwingine” aliagiza Mhe Waziri Ulega