News

FEDHA ZA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA UHURU DESEMBA 9  ZIELEKEZWE KATIKA UKARABATI WA MIUNDOMBINU - MHE WAZIRI MKUU DKT. NCHEMBA

FEDHA ZA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA UHURU DESEMBA 9  ZIELEKEZWE KATIKA UKARABATI WA MIUNDOMBINU - MHE WAZIRI MKUU DKT. NCHEMBA

Dar es Salaam, 24 Novemba, 2025

Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameziagiza taasisi ambazo miundombinu yake imeathirika kutokana na machafuko wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, kufanya tathmini ya kina ya athari zilizojitokeza na kuiwasilisha taarifa ndani ya siku 10 kuanzia tarehe 24 Novemba, 2025, ili serikali iweze kuchukua hatua za haraka.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mbezi Mwisho, wakati akihitimisha ziara yake ya siku moja iliyolenga kukagua uharibifu wa miundombinu na mali jijini Dar es Salaam.

Akiwahutubia wananchi na wadau mbalimbali waliojitokeza, Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Nchemba amesema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma zote za kijamii zilizoathirika zinarejea katika hali yake ya kawaida.

“Ndugu wananchi, kwa niaba ya serikali naomba nianze kwa kutoa pole kwa waathirika wote wa tukio la Oktoba 29, 2025. Ni tukio la kusikitisha na kutafakarisha. Sote tujiulize kwa nini tumefikia hapo,” alisema Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba.

Aidha, Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Nchemba amewaeleza wananchi kuwa kutokana na athari zilizojitokeza, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza maadhimisho ya Sherehe za Uhuru yaliyopangwa kufanyika Desemba 9, 2025 yasitishwe, na badala yake fedha zote zilizotarajiwa kutumika katika maadhimisho hayo zielekezwe kwenye ukarabati wa miundombinu iliyoathirika.

Kuhusu shughuli za ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kazi inaendelea vizuri, ikiwemo ujenzi wa barabara ya kutoka Kibamba kuelekea Mpigi Magohe hadi Bunju yenye urefu wa kilometa 24, pamoja na barabara ya kutoka Kibamba kuelekea Kwembe hadi Makondeko yenye urefu wa kilometa 17.

Halikadhalika, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezielekeza mamlaka zinazohusika na ujenzi wa miundombinu ya barabara kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa wenye sifa ili waweze kutoa mchango wao katika ujenzi wa Taifa.

Awali, akitoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu ya barabara za mwendokasi, Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, alimweleza Waziri Mkuu kuwa zaidi ya shilingi bilioni 12 zinahitajika.