News

ULEGA AAGIZA HATUA ZICHUKULIWE KWA WAKANDARASI WANAOSUASUA KWENYE MIRADI

ULEGA AAGIZA HATUA ZICHUKULIWE KWA WAKANDARASI WANAOSUASUA KWENYE MIRADI

Dodoma, 20 Novemba,2025

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kuwekwa mahabusu na kuandika maelezo kwa wakandarasi wa Kampuni kutoka China First Highway Engineering Co. Ltd, ambao wameshindwa kutimiza masharti ya mkataba wa ujenzi wa barabara, ingawa serikali imetimiwa wajibu wake kwa kulipa sehemu ya malipo.

Ulega amesema pamoja na juhudi za kutaka viongozi wa juu wa kampuni hiyo kutoka China kuja nchini na kutoa maelezo kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa barabara waliyopewa kujenga mkoani Dodoma, zimegonga mwamba hadi sasa na sasa kuna uwezekano wa kuwafikisha mahakamani kwa kukiuka masharti ya mkataba.

Kampuni hiyo ya China First Highway Engineering Co. Ltd. imepewa kazi ya ujenzi wa Sehemu ya pili ya barabara ya Ntyuka- Mvumi Hospitali- Kikombo (Km 53) na ingawa tayari imepewa asilimia 10 ya malipo (kiasi cha shilingi Bilioni 9.68) ujenzi umefikia asilimia mbili pekee.

“Kuanzia sasa hivi, mkandarasi mzembe, mwenye dharau na asiyeendana na ratiba ya mkataba hatutamvumilia na hatua kali za kimkataba zitachukuliwa dhidi yake, sisi tutaendelea kufanya kazi na kuwatumia wakandarasi wanaotimiza majukumu yao lakini wale ambao wamepokea fedha zetu na  hawatimizi upande wao wa mkataba hao tutachukua hatua dhidi yao ili kazi iendelee,” alisema.

Waziri huyo ameagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumshikilia na kumuhoji mkandarasi huyo ambaye alipaswa kufikisha asilimia 13 ya utekelezaji wa mradi huo kufikia sasa hivyo kushindwa kuendana na kasi ya ujenzi licha ya kulipwa fedha kwa wakati.

Aidha, Ulega amesema kuwa licha ya hatua hiyo aliyoichukua pia ataifuatilia miradi mingine inayotekelezwa na mkandarasi huyo na kuahidi kuichukulia hatua zaidi endapo hatoridhishwa na hivyo amemuagiza Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Charles Msonde kuifuatilia kama inaendelea kwa mujibu wa mkataba.

Waziri huyo ambaye pia Mbunge wa Jimbo la Mkuranga amewataka watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha miradi yote inayojengwa inapewa wakandarasi wenye uwezo na wenye uzoefu wa kumaliza miradi kwa wakati.

Amemtaka Mkandarasi CHICO anayejenga sehemu ya Ntyuka- Mvumi- Makulu (Km 8.6) na Kikombo- Chololo – Mapinduzi (Km. 16.4) kuongeza kasi ya ujenzi wa madaraja kabla ya kipindi cha mvua zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.