SERIKALI YAJENGA MADARAJA MAPYA KUUNGANISHA NACHINGWEA NA LIWALE
Lindi, 15 Novemba, 2025
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa madaraja makubwa ya Mbwemkuru II na Nangano katika eneo la Kibukuta, hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto ya mafuriko katika barabara inayounganisha wilaya za Nachingwea na Liwale mkoani Lindi.
Daraja la Mbwemkuru II lina urefu wa mita 64 huku la Nangano likiwa na urefu wa mita 25, na yote yanatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mpango wa dharura wa CERC (Contingency Emergency Response Component) unaolenga kurejesha na kuimarisha miundombinu iliyoathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya kati ya mwaka 2023 na 2024.
Msimamizi wa kazi za ufungaji wa mbao na chuma kwenye daraja la Mbwemkuru II, Joachim Kababa, amesema ujenzi wa madaraja hayo unaendelea vizuri na ukikamilika utaleta afueni kubwa kwa wananchi waliokuwa wakikwamishwa na mafuriko.
Amesema tuta la barabara limeinuliwa na daraja limepanuliwa ili kuruhusu magari mawili kupishana kwa urahisi, tofauti na daraja la awali lililoruhusu gari moja pekee kupita.
Akifafanua zaidi amesema, daraja la zamani liliwahi kufunikwa na maji wakati wa mvua kubwa na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, dereva wa lori la mizigo, Bw. Idrisa Abdallah, ameipongeza serikali kwa ujenzi wa daraja la Mbwemkuru II akisema litapunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa bidhaa wakati wa mvua.
Ameongeza kwa kusema kuwa, madaraja yaliyokuwepo awali yalikuwa hatarishi kwani yakiharibika au maji kuzidi, magari yalilazimika kusimama kwa muda mrefu na kusababisha hasara kwa wasafirishaji.
Naye mkazi wa Kibukuta, Bi. Safina Saidi, amesema madaraja ya zamani hayakuwa na uwezo wa kuhimili maji mengi ya mvua na mara kwa mara mafuriko yaliharibu mazao na mali za wakazi wa eneo hilo.
Akiwa mmoja wa wananchi wanaofaidika na ajira ndogondogo zinazotolewa na mradi huo, amesema ujenzi huo umeleta matumaini mapya kwa jamii ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikikumbwa na athari za mafuriko.
Bw. Yahya Juma kutoka Kijiji cha Nangano amesema kukamilika kwa daraja na kalavati kubwa katika eneo hilo kutarahisisha usafiri wakati wote wa mwaka bila kujali msimu wa mvua au kiangazi na kusisitiza kuwa, kuimarika kwa miundombinu hiyo kutachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo.
Barabara inayounganisha Nachingwea na Liwale ni miongoni mwa barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Lindi, hususan katika usafirishaji wa mazao na huduma za kijamii. Mara kwa mara mafuriko katika maeneo ya Mbwemkuru na Nangano yamekuwa yakisababisha kukatika kwa mawasiliano kwa siku kadhaa, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa madaraja hayo kunatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo.