MAKALAVATI SITA KUONDOA TATIZO LA MAFURIKO KIJIJI CHA MINGUMBI - LINDI
Lindi, 14 Novemba, 2025
Kukamilika kwa ujenzi wa maboksi kalavati sita yanayojengwa kwenye kijiji cha Mingumbi, kupitia miradi ya dharura mkoani wa Lindi yameelezwa yataondoa tatizo la mafuriko ya mara kwa mara yaliyokuwa yakisababishwa na mvua kubwa.
Ujenzi wa miradi ya makalavati hayo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya dharura inayotekelezwa katika mikoa 22 ya Tanzania Bara ukiwemo Lindi, chini ya mpango wa CERC (Contingency Emergency Response Component), ambapo inatekelezwa na makampuni ya wakandarasi wazawa kutoka Tanzania na makampuni kutoka nje ya nchi.
Miradi hii ya maboksi kalavati na barabara katika mkoa huo, kwa mkoa wa Lindi ziliathiriwa pakubwa na mvua za El Niño pamoja na kimbunga Hidaya zilizotokea mwaka 2023 hadi 2024 pamoja na kimbunga Hidaya, vilivyosababisha kukatika kwa mawasiliano na uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Wakazi wa kijiji hicho wameongea kwa nyakati tofauti, huku wakionesha furaha yao kwa ujenzi unaoendelea sasa wa makalavati hayo, ambayo wanaimani kubwa yataondoa na kumaliza kabisa adha ya mafuriko iliyokuwa ikiwapata wakati wa mvua kubwa.
Bi. Fatuma Hassan ambaye ni mamalishe eneo la Mingumbi, amesema kuwa wakati wa mvua kumekuwa hakuna mawasiliano kwenye eneo hilo kutokana na kuzungukwa kwa maji, ila sasa baada ya kukamilika kwa ujenzi huu, maji yaliyokuwa hayana mwelekeo sasa yatakuwa na mwelekeo mmoja tofauti na awali yalikuwa yakisambaa mitaani.
Ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha ujenzi huu, ambao utaondoa adha na shida za kipindi cha mafuriko.
"Kipindi cha mvua kubwa tulikuwa tunajikuta tunakwama sehemu moja maana wengi wetu makazi yetu ni lazima kuvuka mto sasa maji yanakuwa yanajaa sana na tunasubiri hadi yakapungue na yasiupopungua basi tunabaki tulipo kwa masaa kadhaa, ila ninayofuraha kubwa sana ujenzi huu najua ukikamilika shida zetu zitapungua au kuisha kabisa,” amesema Bi. Fatma.
Naye Bw. Mfaume Abdallah, Afisa Usafirishaji, amesema adha kubwa waliyokuwa wakiipata abiria wake ni kushindwa kufika eneo wanalokwenda kwa wakati kutokana na maji kujaa eneo hilo, na endapo wanalazimisha kupita kwenye maji mengi huanguka na chombo kuharibika.
Kwa upande wake, Bi. Vumilia Mpinga, mjasiriamali mkazi wa Mingumbi amesema kipindi cha masika wamekuwa katika hali ya upweke kutokana na maji kujaa sehemu mbalimbali, yaliyokuwa kikwazo cha kuendelea na kazi zao za biashara, na kina mama wanaokwenda kujifungua au kliniki.
“Ilikuwa tukifika hapa kipindi cha masika utakuta wamama tunabebwa na wababa ili tuweze kuvuka hapa kwenda upande wa pili, endapo wapo wanaokwenda kujifungua au kliniki,” amesema Bi. Vumilia.
Naye Bw. Ramadhani Feruzi, mkazi wa Mingumbi amesema sasa wanaimani barabara itakuwa juu kwa kuwa imenyanyuliwa na watafanya shughuli zao vizuri bila bughuza za mafuriko.
“Tunashukuru barabara imenyanyuliwa na madaraja yanajengwa hapa watu walipoteza maisha na mali zao kusombwa na maji yaliyokuwa ni mengi yakitoka milimani,” amesema Bw. Feruzi.