UJENZI WA DARAJA LA LOSINYAI WAFIKIA ASILIMIA 75, HUKU KAZI ZA UJENZI ZIKIONGOZWA NA MKANDARASI MZAWA
Manyara, 06/11/2025
Mradi wa ujenzi wa Daraja la Losinyai unaendelea kwa kasi, ambapo hadi sasa umefikia asilimia 75 ya utekelezaji, huku hatua iliyopo ikiwa ni kumwaga sakafu ya juu (deck).
Akizungumza katika eneo la mradi, Mhandisi wa madaraja kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Makongoro Julius Mwesa, ambaye ndiye msimamizi wa ujenzi huo, amesema daraja hilo lina urefu wa mita 82.4 na upana wa mita 11.2, na linajengwa na mkandarasi wa ndani, kampuni ya Rocktronic Ltd.
Amesema ujenzi huo ulianza baada ya daraja la awali kuharibiwa na mvua kubwa za El-Nino mwaka 2023, ambazo zilisababisha maji kushindwa kupita kwenye mkondo wa kawaida na hivyo kuathiri shughuli za usafiri na uchumi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mwesa, mradi huu unatekelezwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mpango wa dharura wa CERC (Contingency Emergency Response Component), ulioratibiwa na Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mradi huu umetekelezwa kwa miezi 10 sasa, na tunatarajia kuukamilisha ifikapo tarehe 30 Desemba mwaka huu, ndani ya muda wa miezi 12 uliopangwa. Tunafanya kazi kwa viwango vinavyohitajika ili kuhakikisha ubora na uimara wa daraja hili,” alisema Mhandisi Mwesa.
Daraja la Losinyai lina umuhimu mkubwa wa kiuchumi kwani linaunganisha Mkoa wa Manyara (Wilaya ya Simanjiro) na Jiji la Arusha, hivyo kurahisisha usafirishaji wa mazao kama mahindi, maharage, alizeti, pamoja na mifugo kutoka maeneo ya Simanjiro, Kiteto na hata Dodoma kuelekea Arusha.
Mbali na hilo, mradi huu umeleta ajira kwa wananchi wa maeneo jirani, ambapo jumla ya vijana 60 wamepata ajira rasmi huku wanaume wakiwa 50 na wanawake 10 na wengine wakijipatia ajira zisizo rasmi kama mama lishe wanaotoa huduma za chakula kwa wafanyakazi wa mradi.
Kwa upande wake, Mhandisi msimamizi wa ujenzi David Sanagala kutoka kampuni ya Rocktronic Ltd, ametoa shukran zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
“Tunatekeleza kazi hii kwa kufuata masharti ya mkataba, tukizingatia ubora, muda na bajeti. Ajira tulizopata zimekuwa msaada mkubwa kwetu na familia zetu. Tunaomba Serikali iendelee kutuamini ili tuweze kuongeza ujuzi na kuinua kipato chetu,” alisema Sanagala.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Mwesa ametoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na eneo la mradi kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu hiyo, akisisitiza kuwa daraja hilo litakuwa chachu ya maendeleo kwao na kwa Taifa kwa ujumla.