BARABARA YA DODOMA - IRINGA ENEO LA FUFU YAFUNGULIWA RASMI BAADA YA UKARABATI
Dodoma, 16 Oktoba, 2025
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imekamilisha ujenzi wa barabara ya Dodoma - Iringa eneo la Fufu uliogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 8.7 kwa kunyanyua tuta la barabara lenye urefu wa kilomita 4 na kujenga makalvati makubwa manne.
Barabara hiyo imefunguliwa rasmi kuanza kutumika tarehe 16 Oktoba, 2025 na Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo wa dharura umezingatia viwango vya ubora ili kuondoa changamoto iliyokuwepo hapo awali ya kujaa maji na kusababisha adha kwa wasafiri na wasafirishaji.
”Tumekamilisha ujenzi wa barabara ya kipande cha Fufu kilichokuwa kinajaa sana maji, kutokana na makalvati yaliyokuwepo awali yalikuwa madogo, ambayo yalishindwa kupitisha maji na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara hii, kwa kukaa saa kadhaa ili kusubiri maji yapungue na waweze kupita”, ameeleza Mhandisi Zuhura.
Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa barabara hiyo imejengwa na mkandarasi mzawa kampuni ya GNSM Contractors Limited kwa mkataba wa mwaka mmoja na mpaka sasa imekamilika kwa asilimia 97 na kazi zilizobakia ni uwekaji wa alama za barabarani pamoja na kingo za barabara.
Aidha, Mhandisi Zuhura ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuona umuhimu wa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya dharura ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 kiasi cha Shilingi Bilioni 35.6 zilitengwa.
Kwa upande wa wananchi wa kijiji cha Fufu wameipongeza Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao utachochea biashara na pia wameomba kuwekewa kivuko cha kuvusha mifugo pamoja na kujenga mitaro ili kuruhusu maji yaweze kupita kwa urahisi, hadi kwenye makalvati mapya yakiyojengwa na kutosababisha uharibu tena wa maji katika kijiji cha Gezaulole.
Naye, Dereva wa magari makubwa anayetumia barabara hiyo Bw. Juli Daudi ameishukuru serikali kwa ujenzi huo sasa itawaondolea adha ya kupita kwa muda mrefu katika barabara ya changarawe ya mchepuo, ambapo walikuwa wakitumia dakika 35 hadi 40 na sasa hivi watatumia dakika 5 hadi 10.