News

TANROADS NA BENKI YA DUNIA WAWEKA SULUHISHO LA KUDUMU LA MAFURIKO YA KIJIJI CHA IDODI

TANROADS NA BENKI YA DUNIA WAWEKA SULUHISHO LA KUDUMU LA MAFURIKO YA KIJIJI CHA IDODI

Dar es Salaam, 15 Oktoba, 2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia kwa mhandisi mshauri wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa-Msemba Kilometa 104 wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha upembuzi yakinifu wa ujenzi huo, ambapo sasa wanakuja na suluhisho la kudumu la kuondoa mafuriko kwenye kijiji cha Idodi.

Mhandisi Mshauri, Dkt. Magayane Machibya, ambaye anafanya upande wa mafuriko na maji amesema hayo leo tarehe 15 Oktoba, 2025, wakati akiwasilisha upembuzi yakinifu huo mbele ya wadhamini wa mradi huo Benki ya Dunia uliopo chini ya mpango wa Tanzania Transport Integration Project (TanTip), ambao unalenga kuboresha mtandao wa usafiri nchini kwa kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko kupitia barabara za kisasa zenye viwango vya kimataifa.

Mha. Dkt. Machibya amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara pamoja na madaraja na makalavati, ambapo kwa upande wa udhibiti wa mafuriko kwenye kijiji cha Idodi, katika upembuzi huo wameweka mikakati mikubwa mitano ya kunyanyua na kujenga daraja kubwa litakalopitisha maji kwa urahisi tofauti na la awali lilikuwa chini na wakati wa mvua kubwa michanga na uchafu ilijaa na kusababisha maji kupita juu ya daraja la kusambaa kwa wakazi wa eneo hilo; pia mkakati mwingine ni kutengeneza mifereji mikubwa itakayokuwa ikitoa maji kwenye bwawa la Nsunda na kuyapeleka kwenye mto Idodi.

Pia amesema mkakati mwingine ni kujenga kalavati kubwa litakalokuwa likipeleka maji kwenye mto Msimbi, awali daraja lililokuwepo lilikuwa dogo na kufanya maji kusambaa kwa wakazi wa eneo hilo; pia kutafanyika zoezi la mara kwa mara la kusafisha mto Idodi kwa kuondoa mchanga na chanzo cha mchanga kwa kuchepusha mto na kuupeleka kwenye eneo lisilokuwa na udongo tifutifu, kwani awali mto huo ulikuwa ukipita kwenye eneo hilo na kusababisha kukaa kwa muda mrefu.

Pia amesema wataweka kalvati mbili kubwa eneo la Makondeko ambalo kunafanyika kilimo cha umwagiliaji, ambayo yatakuwa sambamba na ujenzi wa mifereji mikubwa mitatu itakayokuwa inajitegemea kila mmoja, tofauti na awali maji yalikuwa yakisambaa bila mwelekeo.