News

WAFANYAKAZI WA TANROADS KANDA YA MASHARIKI WAONGOZA KWA KUHAMASISHA MAZOEZI YA MWILI

WAFANYAKAZI WA TANROADS KANDA YA MASHARIKI WAONGOZA KWA KUHAMASISHA MAZOEZI YA MWILI

Dar es Salaam, 11 Oktoba 2025 

Wafanyakazi wanaounda timu za mpira wa miguu, netiboli na kuvutana kamba za Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Kanda ya Mashariki wamewahimiza watumishi wenzao kote nchini kuzingatia mazoezi ya mara kwa mara ili kujenga afya bora, kuimarisha utendaji kazi na kuongeza mshikamano katika maeneo ya kazi. 

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa TANROADS Kanda ya Mashariki, Bw. Twahir Salim, wakati wa mchezo wa kirafiki kati ya timu ya TANROADS East Zone na Nyika Veterans kutoka Pwani, uliochezwa katika Uwanja wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), Kunduchi. Katika mchezo huo wa kuvutia, TANROADS East Zone walishinda kwa mabao 4–3, yakifungwa na Mselemu Ramadhani, Charles Ndetabula, Mabula Andrew, na Gabriel Bazil, huku wapinzani wao wakifunga kupitia Silvester Mgonafizi, Inga Abdallah, na Gwamaka Mwambusi.

 Bw. Twahir alieleza kuwa timu hiyo imekuwa ikifanya mazoezi ya pamoja kila Jumamosi katika uwanja huo wa NDC kama sehemu ya kuimarisha afya, kuongeza uimara wa mwili na kuboresha umakini kazini.

“Sisi ni kawaida yetu kufanya mazoezi ya pamoja kila Jumamosi lakini kwa siku za kazi kila mmoja wetu anafanya mazoezi binafsi, kwa kuwa hii timu inaundwa na wachezaji wanaotoka TANROADS Pwani yaani Kibaha, Ikwiriri, Kibiti, Tumbi, na Dar es Salaam kwa siku za kazi inakuwa ngumu kukutana pamoja, lakini kwa Jumamosi wanakuwepo na baadhi wanaokuwa kwenye majukumu nje ya mkoa wanaendelea na mazoezi walipo,” alisema Bw. Twahir.

Aidha, aliuomba uongozi wa TANROADS kuendelea kuwasaidia katika gharama za uendeshaji wa timu ikiwemo malipo ya uwanja, maji, vifaa vya michezo kama mipira na jezi, dawa za matibabu na usafiri wa wachezaji, akibainisha kuwa kwa sasa wanajitolea kuchangia gharama hizo wenyewe.

“Lengo letu ni kujenga afya bora, kuimarisha akili na kuzuia magonjwa nyemelezi, ili tuendelee kutoa huduma bora kwa wananchi,” aliongeza.

Kwa upande wake, Kocha na Mchezaji wa timu ya Nyika Veterans, Afande Silvester Mgonafizi, kutoka Makao Makuu ya Kamandi ya Kibaha Msangani, alisema mazoezi ni sehemu ya maisha ya wanajeshi na yanasaidia kuongeza ufanisi katika kazi za kila siku.

“Tunakaribisha timu zingine, zikiwemo za taasisi za umma na binafsi, kuungana nasi katika michezo ya kirafiki kama njia ya kujenga afya na undugu,” alisema Afande Mgonafizi.