TANROADS na LEA Wapitia Marejeo ya Usanifu wa Barabara ya Rutukila – Songea
Dar es Salaam, 07 Oktoba 2025
Wahandisi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) leo tarehe 7 Oktoba 2025 wamefanya kikao cha kazi na wataalam kutoka Kampuni ya LEA International Ltd ya Canada, kwa kushirikiana na LEA Associates South Asia Pvt Ltd ya India pamoja na Howard Consulting Ltd ya Tanzania, kwa ajili ya kupitia marejeo ya usanifu (Design Review) wa barabara ya Rutukila – Songea, yenye urefu wa kilomita 116.
Barabara hii ni miongoni mwa miradi saba mikubwa inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank) chini ya mpango wa Tanzania Transport Integration Project (TANTIP), ambao unalenga kuboresha mtandao wa usafiri nchini kwa kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko kupitia barabara za kisasa zenye viwango vya kimataifa.
Kupitia kikao hiki, wataalam wa TANROADS na LEA wamejadili kwa kina vipengele vya kiufundi, usanifu wa miundombinu ya barabara, ubora wa vifaa vitakavyotumika, na hatua za kuhakikisha ujenzi unazingatia viwango vya kimataifa vya ubora, usalama na uendelevu wa mazingira.
Mradi wa barabara ya Rutukila – Songea unatarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Ruvuma kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao, bidhaa na huduma, pamoja na kuongeza fursa za ajira wakati wa ujenzi na baada ya kukamilika kwake.
TANROADS inaendelea kushirikiana kwa karibu na washirika wa maendeleo kama Benki ya Dunia na makampuni ya kitaalam kuhakikisha miradi yote chini ya mpango wa TANTIP inatekelezwa kwa ufanisi, kwa wakati, na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.