TANROADS NA BENKI YA DUNIA WAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MIRADI YA TANTIPS
Dar es Salaam, 06 Oktoba 2025
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kupitia Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongeza ushirikiano thabiti kati yake na Benki ya Dunia katika kufadhili na kusimamia utekelezaji wa miradi saba ya maendeleo ya miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege katika baadhi ya mikoa nchini.
Akizungumza leo tarehe 06 Oktoba 2025 katika kikao cha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi inayoendelea chini ya programu ya Tanzania Transport Integration Project (TANTIP), Mkurugenzi wa Miradi ya Maendeleo wa TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko, alisema ushirikiano huo ni mfano bora wa namna Tanzania na Benki ya Dunia wanavyotekeleza miradi ya kimkakati kwa pamoja ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhandisi Nnko alieleza kuwa miradi hiyo saba inafadhiliwa kwa jumla ya Dola za Marekani milioni 550, sawa na shilingi trilioni 1.3 za Kitanzania, ambapo miradi minne inahusu barabara na miradi mitatu ni ya viwanja vya ndege.
Ameitaja miradi ya barabara hiyo kuwa ni:
Lusaunga – Rusumo (Km 92) mkoani Kagera;
Iringa – Msembe (Km 104) mkoani Iringa;
Mtwara – Mingoyo – Masasi (Km 206), iliyogawanywa katika sehemu mbili: Mtwara–Mingoyo na Mingoyo–Masasi;
Rutukila – Songea (Km 116) pamoja na kipande cha mchepuko, ambapo kandarasi ya ujenzi inatarajiwa kusainiwa hivi karibuni.
Kwa upande wa miradi ya viwanja vya ndege, Mhandisi Nnko alitaja kuwa inahusisha Kiwanja cha Ndege cha Tanga, Lake Manyara, na Iringa. Alifafanua kuwa kwa viwanja vya Tanga na Lake Manyara, kazi zinazofanyika ni ujenzi wa barabara za kurukia na kutua ndege, pamoja na majengo ya abiria na majengo saidizi. Kwa Kiwanja cha Ndege cha Iringa, ujenzi unaendelea katika jengo la abiria, huku barabara ya kurukia na kutua ndege pamoja na majengo saidizi yakiwa tayari yalijengwa na Serikali.
Mhandisi Nnko aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umetoa ajira zaidi ya 1,300 kwa Watanzania, ambapo wanaume ni 976 (asilimia 75) na wanawake 325 (asilimia 25). Idadi hii, alisema, inatarajiwa kuongezeka pindi miradi mingine iliyo katika hatua za manunuzi itakapoanza rasmi.
Mhandisi Nnko alisema TANROADS inatambua umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa kimkakati na washirika wa maendeleo kama Benki ya Dunia, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuhakikisha miradi ya miundombinu inachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Aliongeza kuwa mazungumzo yanaendelea kuhusu uwezekano wa kuongeza ufadhili hasa katika ukarabati wa barabara ili kuongeza muda wake wa matumizi na kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hii kutachochea ukuaji wa uchumi hususan katika mikoa ya kusini ya Ruvuma na Mtwara, ambako shughuli za kiuchumi na uwekezaji mkubwa zinaendelea.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendeleza uhusiano mzuri na mashirika ya maendeleo, jambo alilosema linachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha miundombinu nchini. Alibainisha kuwa miradi yote ya TANTIP inatarajiwa kukamilika mwaka 2027.