MRADI WA UJENZI WA BOXCULVERT DABIL WAFIKIA ASILIMIA 98
Babati
29 Oktoba, 2025
Mradi wa ujenzi wa boxculvert katika eneo la Dabil, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, umefikia asilimia 98 ya utekelezaji na umeanza kutumika na watumiaji wa barabara hiyo, hatua inayoelezwa sasa itaondoa changamoto ya maporomoko ya mawe yaliyokuwa yakisababisha usumbufu katika eneo hilo.
Mradi huo ulianza Novemba 2024 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na unatekelezwa na mkandarasi Madata Investment Ltd chini ya usimamizi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Manyara.
Kwa muda mrefu, wananchi wa Dabil walikuwa wakikabiliwa na maporomoko ya mawe kutoka mlimani, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama na kusababisha kufungwa kwa barabara. Kukamilika kwa boxculvert hiyo kumewezesha magari na watumiaji wengine kuanza kupita bila kikwazo.
Wakizungumza kwa niaba ya wananchi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameishukuru Serikali na TANROADS kwa juhudi za kufanikisha mradi huo, wakibainisha kuwa umerejesha mawasiliano na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Aidha, wananchi hao wamepongeza ushirikiano uliokuwepo kati ya Ofisi ya Meneja wa TANROADS mkoa wa Manyara na mkandarasi, hatua iliyowezesha mradi huo kufikia ukamilifu kwa wakati.