News

WAKAZI SIMIYU WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA DARAJA LA SIMIYU

WAKAZI SIMIYU WAISHUKURU SERIKALI KWA UJENZI WA DARAJA LA SIMIYU

16 Septemba, 2025

Simiyu

Wakazi wa Mkoa wa Simiyu wameishukuru Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ujenzi wa daraja jipya la Simiyu, wakieleza kuwa kukamilika kwake kutamaliza kero ya mafuriko yaliyokuwa yakiwasumbua mara kwa mara wakati wa mvua kubwa.

Bw. Juma Joseph, mkazi wa Kisamba, alisema awali magari yalikuwa yakikwama kwa muda mrefu kutokana na maji mengi kufunika daraja na kusambaa kwenye makazi na mashamba ya wananchi.

Alisema: “Tunashukuru sana Serikali kwa ujenzi huu. Tunaamini sasa unakwenda kutatua kero kubwa ya mafuriko. Kwa mfano, mwaka 2000 maji ya mvua yalikuwa mengi sana na kusababisha mafuriko kwa sababu hayakupita vizuri kwenye matundu ya daraja. Sasa kwa ujenzi huu hatuna shaka tena. Hata hivyo, tunaomba pia ufanyike upanuzi wa mto ili maji yapite kwa urahisi zaidi.”

Naye Bw. Twaha Nassib alisema daraja hilo litakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kwa kuwa awali wakati wa masika maji mengi yalikuwa yakipita juu ya daraja na kuzuia magari, mifugo na watumiaji wengine kuvuka.

“Ninaishukuru Serikali, lakini pia naomba madaraja mengine katika Simiyu na maeneo mengine nchini yawekwe kwenye mpango wa ukarabati ili wananchi waweze kusafiri kwa wakati wanapokwenda kwenye shughuli zao za kujiongezea kipato,” alisema Bw. Nassib.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Kampuni ya CCECC, Bw. Gervas Robert, alisema daraja hilo limepanuliwa na sasa litakuwa na urefu wa mita 175 na upana wa mita 12.5, hatua itakayoruhusu magari mawili kupishana kwa wakati tofauti na awali ambapo gari moja pekee lililazimika kusubiri lingine lipite.

Aliongeza kuwa mradi huo pia unajumuisha ujenzi wa barabara unganishi zenye jumla ya urefu wa kilometa 3, ikiwemo kilometa 1.8 upande wa Mwanza na kilometa 1.2 upande wa Simiyu.

“Hadi sasa tumekamilisha usukaji wa nguzo mlalo 25 na ujenzi umefikia asilimia 62. Mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 2026. Tunawashukuru Serikali kwa mradi huu kwa sababu utapunguza changamoto ya msongamano wa magari, hasa kwa kuwa daraja hili hutumika pia na magari kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda,” alisema Mhandisi Robert.

Alifafanua kuwa mradi huo unahusisha wafanyakazi 175, wakiwemo wazawa na wataalamu kutoka China.