News

WASHIRIKI SHIMIWI WAIPONGEZA SERIKALI UJENZI WA DARAJA LA JPM MWANZA

WASHIRIKI SHIMIWI WAIPONGEZA SERIKALI UJENZI WA DARAJA LA JPM MWANZA

Mwanza12 Sept, 2025

Washiriki wa michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), wameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa daraja la JPM linaloanzia eneo la Kigongo hadi Busisi jijini Mwanza.

Washiriki hao takribani 2000 kutoka klabu mbalimbali wamefanya utalii wa ndani kwenye daraja hilo, ikiwa ni siku moja imetengwa kwenye ratiba ya  michezo ya SHIMIWI inayoendelea jijini Mwanza kutembelea vivutio vya utalii kwenye mkoa husika na mikoa ya jirani.

Katibu wa klabu  ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Patrick Kutondolana amesema serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imefanya uwekazaji mkubwa unaounganisha Tanzania na nchi jirani za Kenya na Uganda

Bw. Kutondolana amesema kuwa daraja hili litakuza uchumi katika sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii, usafiri na usafirishaji, kwa kuwa sasa limerahisisha usafiri, lakini ametoa wito kwa serikali kutoa taratibu zaidi za matumizi ya daraja hilo ikiwemo ya wananchi kuruhusiwa kupiga picha za matukio mbalimbali ya harusi na kipaimara.

Naye Bw. Levo Basil, anatokea Bunge SC amesema daraja hili linaokoa muda wa watuamaji wa daraja hili, ambapo utakuza uchumi, lakini ametoa wito kwa serikali kuangalie uwezekano wa kuweka ada ndogo kwa wanatumiaji wa daraja hili ilii liweze kurudisha gharama za ujenzi.

Kwa upande wake Bw. Nsekela Majuto, Katibu  wa klabu ya RAS Dodoma amesema washiriki wamejivunia, kufurahia na kufarijika kuona serikali inatekeleza miradi mikubwa, inayoweka alama. 

Katibu mkuu wa Klabu ya Michezo ya wizara ya Ujenzi, Bi. Mary Sudi ametoa kongole kubwa kwa serikali kwa kufanikisha mradi huu kwa asilimia 100, kwani daraja hili ni la pekee kwani litaleta mafanikio makubwa kwa nchi.

Bw. Festo Mgata, katibu wa klabu ya wizara ya Afya amesema wanajivunia kwa mradi huu, kwani umeleta mabadiliko chanya na mfano mzuri ni usafiri wa awali kabla ya kujengwa kwa daraja kulikuwa na msongamano wa watuamiaji wa kivuko kilichokuwa kikiwatoa Mwanza eneo la Busisi na kuwapeleka Kigongo.

Naye Innocent George wa Klabu ya Wizara ya Katiba na Sheria, amesema daraja hili nikiunganisihi kati ya jiji la Mwanza na Wilaya ya Sengerea.

Awali Mhandisi msimamizi wa daraja hilo, Aloyce Kado amesema ujenzi wa daraja hili ulianza February 2020 na kumalizika 29 Mei, 2025 daraja hili linaurefu wa Km 3 na barabara unganishi zenye urefu wa Km.1.66, na litafungwa kamera za usalama ili kubaini wenye kufanya uhalifu.

Mha. Kado ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ujenzi wa daraja hili, na ametoa wito ihakikishe inatekeleza miradi mingine kama huu ili kurahisisha usafiri kwa watumiaji wake. 

Mbali na washiriki kufanya utalii wa ndani kwenye daraja la JPM, pia baadhi yao walitembelea Butiama kwenye kaburi la hayati Rais Mstaafu Mwl. Julius Kambarage Nyerere, mbuga za wanyama za Serengeti na Kisiwa cha Saanane.