DARAJA JIPYA LA MKUYUNI MWANZA KUONDOA KERO YA MAFURIKO
Mwanza, 12 Septemba 2025
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inatekeleza ujenzi wa daraja jipya eneo la Mkuyuni jijini Mwanza, mradi unaotarajiwa kuwa suluhisho la tatizo la mafuriko yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara pindi mvua kubwa zinaponyesha.
Daraja hili lina upana wa mita 15 na njia sita. Ujenzi ulianza Novemba 13, 2024 na unatarajiwa kukamilika Novemba 13, 2025 chini ya usimamizi wa mkandarasi mzawa Jasco Co. Ltd. Awali, eneo hilo lilikuwa na boksi kalavati moja ambalo lilishindwa kuhimili wingi wa maji yaliyokuwa yakijaa na kuchanganyika na taka, hali iliyosababisha athari kubwa kwa makazi na miundombinu ya usafirishaji.
Mhandisi Ipimilo Dwasi wa Jasco Co. Ltd alibainisha kuwa mkandarasi ameweka utaratibu wa kufanya kazi kwa zamu mchana na usiku, kila zamu ikihusisha wafanyakazi 25. Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kabla ya mvua za masika kuanza. Aliongeza kuwa serikali imetoa fedha kwa wakati, jambo lililowezesha kazi kuendelea bila kusimama.
Mradi huu umeleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii. Zaidi ya watu 100 wamepata ajira na wajasiriamali wadogo wa eneo hilo wameongeza kipato kutokana na mahitaji ya bidhaa na huduma zinazotokana na ujenzi.
Mkazi wa Mkuyuni, Mussa Jacob, alieleza kuwa tatizo la kukatika kwa mawasiliano kati ya Nyegezi na katikati ya jiji kutokana na maji kujaa litabaki historia. Alisisitiza kuwa ujenzi huu utaongeza ufanisi wa shughuli za kila siku na kuimarisha vipato vya wananchi.
Naye mkazi mwingine, Coline Kahanda, alisema kuwa usumbufu wa magari kukwama au kuahirishwa safari wakati wa mvua kubwa hautakuwepo tena baada ya kukamilika kwa daraja hilo.
Faida za mradi huu zimefika pia kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Christina Shinzeh, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Uhandisi kutoka Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), anayefanya mafunzo kwa vitendo TANROADS Mwanza, alisema mradi huo umemsaidia kujifunza uhalisia wa kazi za uhandisi ambao darasani hujifunza kwa nadharia zaidi.
Kwa upande wake, Mhandisi Yasinta Charles kutoka Jasco Co. Ltd alieleza kuwa kampuni hiyo imedhamiria kukamilisha kazi kwa viwango vya juu kama masharti ya mkataba yanavyotaka na akaipongeza serikali kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa.