News

BARABARA YA MNIVATA-MASASI YAPIGA HATUA KUBWA YA UJENZI, YATARAJIWA KUIMARISHA UCHUMI

BARABARA YA MNIVATA-MASASI YAPIGA HATUA KUBWA YA UJENZI, YATARAJIWA KUIMARISHA UCHUMI

Mtwara,

07/09/2025

Mradi wa ujenzi wa barabara ya kimkakati ya Mnivata–Masasi yenye urefu wa kilomita 160 kwa kiwango cha lami unaendelea kwa kasi, ambapo sehemu kubwa ya kazi muhimu za awali na msingi wa barabara tayari zimekamilika, hadi sasa, mafanikio makubwa yamepatikana katika ujenzi wa tuta, madaraja makubwa na madogo pamoja na maandalizi ya tabaka la saruji kwa ajili ya kuweka lami.

Utekelezaji wa mradi huu umegawanyika katika sehemu mbili: kipande cha Mnivata–Mitesa (Km 100) na Mitesa–Masasi (Km 60), ambako kazi za ujenzi zimepiga hatua kubwa na zinaendelea kwa kasi, hali inayoonesha dhamira ya kukamilisha mradi huu kwa wakati uliopangwa.

Mradi huu, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 270.9, unafadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inayochangia sehemu kubwa ya fedha, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kwa upande wa utekelezaji, kampuni za kimataifa na za ndani zimepewa jukumu la usimamizi na ujenzi, hatua inayohakikisha viwango vya ubora na ushirikiano wa kitaalam unaofanikisha utekelezaji.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto Chacha John, ameeleza kuwa mradi huu utarahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kama korosho, ufuta na mahindi, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji kupitia Mtwara Development Corridor, na kuboresha huduma muhimu za kijamii ikiwemo elimu na afya.

Aidha, mradi umetoa fursa za ajira kwa wakazi wa maeneo unaopitia, hatua inayoongeza kipato na kuimarisha ustawi wa familia. Kwa ujumla, barabara ya Mnivata–Masasi inatajwa kuwa kituo cha maendeleo mapya kwa ukanda wa Kusini, na kukamilika kwake kutaimarisha uchumi na ustawi wa taifa kwa ujumla.