VIONGOZI WA TANROADS WANUFAIKA NA MAFUNZO YA UONGOZI
Morogoro
28 Agosti, 2025
Menejimenti na Mameneja wa mikoa wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wameshiriki mafunzo maalum ya uongozi yaliyolenga kuwajengea uwezo, kuimarisha weledi, na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo, yaliyoandaliwa kwa umakini na kitaalamu, yamefanyika mkoani Morogoro kwa kutumia mbinu shirikishi zinazowezesha washiriki kushiriki kikamilifu badala ya kusikiliza pekee.
Washiriki walipitia mazoezi ya vitendo kama vile michezo ya mafunzo kupitia karata na mpangilio wa vitu, ambayo ilitumika kufundisha umuhimu wa mawasiliano, mshikamano wa timu, na kupanga mikakati ya pamoja, kupitia njia hizi, watumishi walipata uzoefu wa moja kwa moja kuhusu namna bora ya kushughulikia changamoto, kufanya maamuzi ya haraka, na kuongeza mshikamanio katika kazi za kila siku.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Muwezeshaji kutoka Chuo cha Uongozi, Fortunatus Ekklesiah, alisema mbinu shirikishi ni nyenzo yenye ufanisi mkubwa katika kuongeza uelewa wa washiriki.
“Mafunzo haya yamekusudia kuchochea ubunifu, kuimarisha ushirikiano, na kuwapa washiriki stadi za kutatua changamoto za kikazi kwa haraka na kwa ufanisi,” alisisitiza.
Washiriki wa mafunzo walieleza kuwa yamewapa mtazamo mpya wa kiuongozi, hususan katika kushirikiana, kuongoza timu kwa ufanisi, na kuboresha maamuzi kwa kuzingatia maadili na weledi. Wamepongeza TANROADS kwa kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya kujenga uwezo ambayo ni msingi wa usimamizi bora wa miradi mikubwa ya miundombinu ya barabara nchini.
Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia TANROADS wa kuhakikisha viongozi na mameneja wake wanakuwa na maarifa, stadi na mbinu za kiuongozi zinazohitajika kusimamia utekelezaji wa miradi ya kitaifa kwa viwango vinavyokidhi malengo ya maendeleo endelevu ya Taifa.