SERIKALI YATOA BIL. 36.5 UJENZI WA MIRADI YA DHARURA DODOMA
Dodoma
28 Agosti, 2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha shilingi Bililioni 35.6 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya dharura ya mkoani Dodoma.
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani amesema fedha hizo zimelengwa kutumika katika miradi mitano ya dharura baada ya kuharibika kwa barabara, madaraja na makalavati katika kipindi cha mvua kubwa za el-nino zilizotokea nchini mwaka 2023 hadi 2024.
Mha, Zuhura amesema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa miradi mitano ya dharura, ambayo ni Mbande, Morena, Fufu, Nzali-Chilonwa, Silwa - Pandambili.
Amesema miradi hii inatekeleza ujenzi wa vipande vya barabara vilivyoathirika, na kujengwa kwa madaraja na kuongeza makalavati makubwa ambayo yatasaidia kupita kwa maji kwa wingi.
Mha. Zuhura amesema tayari wamewaelekeza wakandarasi wote juu ya umuhimu wa miradi hii kuhakikisha wanafanya kazi kwa muda wa ziada, ili kufikia matarajio ya kukamilika mapema mwishoni mwa mwezi wa Oktoba.
“Mikataba inawataka wakandarasi wote waliopewa miradi hii kukamilisha mapema ili kuziwahi mvua zitakazoanza mwezi Novemba, maana mkoa wetu huu umekuwa na mvua nyingi kipindii hiki, hivyo ninaimani na tunatarajia kazi hizi zitakamilika kwa wakati,” amesema Mha. Zuhura.
Hatahivyo, Mha. Zuhura ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha zote za ujenzi wa miradi hiyo ya dharura.
Mbali na miradi hii ya dharura, wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS inaendelea na ujenzi wa miradii ya kimkakati ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato pamoja na barabara ya mzunguko wa nje.