TANROADS YASISITIZWA UBUNIFU NA UWAJIBIKAJI
Morogoro
26 AGOSTI, 2025
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, amewataka viongozi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuendeleza ubunifu, weledi na uwajibikaji katika usimamizi wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara nchini. Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kutekeleza kwa ufanisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga miundombinu bora na ya kisasa itakayochochea maendeleo ya Taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa Menejimenti na Mameneja wa TANROADS, Balozi Mhandisi Amour alisisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika sekta ya miundombinu. Alibainisha kuwa viongozi wa TANROADS wanapaswa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora wa juu na kukamilika kwa wakati.
Aidha, Balozi Mhandisi Amour alieleza kuwa viongozi hao wanapaswa kuwa wabunifu na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na sayansi duniani, ili kuongeza tija katika sekta ya barabara. Aliongeza kuwa wajibu mkubwa uko mikononi mwao kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa ufanisi, kwa kuzingatia uwazi, matumizi bora na uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa maafisa wake waandamizi. Alifafanua kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi kwa viwango vilivyokusudiwa.
Mhandisi Besta aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza maarifa, ufanisi na uwezo wa viongozi wa TANROADS katika ngazi za mikoa, na yatakuwa chachu ya mabadiliko chanya katika utendaji wao wa kazi, hivyo kusaidia Serikali kufikia malengo ya kukuza uchumi kupitia sekta ya miundombinu.