TANROADS YAIMARISHA USIMAMIZI WA FEDHA KUPITIA MAFUNZO YA MFUMO WA MUSE
Morogoro
23/8/2025
MOROGORO, 22 Agosti 2025 – Menejimenti na Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wamehitimisha mafunzo maalum ya mfumo wa kisasa wa kifedha wa MUSE (Mfumo wa Ulipaji Serikalini) yaliyotolewa na Wizara ya Fedha, kwa lengo la kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa rasilimali fedha za umma.
Mafunzo hayo, yaliyofanyika katika ukumbi wa NSSF mkoani Morogoro kuanzia tarehe 21 hadi 22 Agosti 2025, yamekusudia kuhakikisha usimamizi madhubuti wa fedha katika miradi mikubwa ya miundombinu inayosimamiwa na TANROADS ikiwemo barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko alieleza kuwa taasisi imejipanga kikamilifu kuhamia rasmi katika mfumo wa MUSE kutoka mfumo wa zamani wa EPICOR, ili kuongeza uwajibikaji na kuimarisha nidhamu ya kifedha.
Mwenyekiti wa Mafunzo na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Ujenzi, Ndugu Jamal Gwakisa Brown, alieleza kuwa MUSE ni mfumo kamili unaojumuisha vipengele vyote muhimu vya usimamizi wa fedha na kwamba washiriki wameonesha dhamira thabiti katika kuukubali mfumo huu mpya. Alisisitiza kuwa MUSE ni suluhisho la changamoto za usimamizi wa fedha na unatarajiwa kuongeza ufanisi na mageuzi katika sekta ya umma.
Bi. Mariana Lamosai, Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo ya Fedha Wizara ya Fedha, alibainisha kuwa matumizi ya MUSE yatasaidia kuimarisha uaminifu wa kifedha na kuhamasisha ushiriki wa wawekezaji pamoja na wadau wa maendeleo. Alisisitiza kuwa mfumo huu utaleta uwazi na imani katika usimamizi wa fedha za serikali na hivyo kurahisisha upatikanaji wa rasilimali kwa miradi ya miundombinu.
Mafunzo hayo yamewezeshwa pia na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha, akiwemo CPA Lilian Kajubiri (Mhasibu Mkuu Wizara ya Ujenzi), Bw. Emmanuel Mapande (Mchumi, Wizara ya Ujenzi), na Bw. Francis Fungameza (Mwezeshaji Wizara ya Fedha), ambapo washiriki walipewa mwongozo wa kitaalamu kuhusu namna mfumo wa MUSE unavyoweza kuongeza uwajibikaji na kupunguza changamoto katika utekelezaji wa bajeti za maendeleo.
Kwa ujumla, mafunzo haya yamekuwa hatua muhimu katika safari ya TANROADS ya kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwazi na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali kwa ajili ya ustawi endelevu wa taifa.