AFYA BORA YA WATUMISHI, MSINGI WA UFANISI – TANROADS KILIMANJARO YAONGOZA NJIA
Kilimanjaro
23/8/2025
Ofisi ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro imekuwa mfano bora wa kuonyesha namna afya njema ya watumishi inavyokuwa msingi wa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakala wa Barabara Tanzania. Kutambua umuhimu huo, menejimenti ya Mkoa imeanzisha na kuendesha programu endelevu ya kufanya mazoezi ya viungo kila wiki, ikiwashirikisha watumishi wote katika ofisi hiyo.
Mazoezi haya hufanyika katika viwanja vya Ofisi ya Meneja wa Mkoa na yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha afya za watumishi, kujenga mshikamano, pamoja na kuongeza morali na ufanisi wa kazi. Hatua hii imedhihirisha uongozi thabiti wa Menejimenti ya Mkoa wa Kilimanjaro katika kuhakikisha kuwa watumishi wanakuwa na afya bora ili kutimiza malengo ya taasisi kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.
Zaidi ya kuimarisha afya za watumishi wake, Ofisi ya Meneja wa Mkoa imepanua wigo wa mazoezi hayo kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma. Hatua hii imejenga mshikamano wa kijamii na kudumisha uhusiano mwema baina ya taasisi. Mnamo tarehe 21 Agosti 2025, Mahakama Kuu Kanda ya Kilimanjaro pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) walishiriki kikamilifu katika mazoezi ya pamoja yaliyoandaliwa na Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa TANROADS Kilimanjaro.
Kwa hatua hii, TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro si tu imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kusimamia miundombinu ya barabara, bali pia imeonesha mfano wa kuigwa katika kujali ustawi na afya ya watumishi wake kama nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi wa kiutendaji.