News

TANROADS YATOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WANAFUNZI NA WAENDESHA BODABODA

TANROADS YATOA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WANAFUNZI NA WAENDESHA BODABODA

Dodoma

22/08/2025

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeendesha kampeni maalum ya elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza ajali na kuhakikisha matumizi salama ya barabara nchini.

Kampeni hiyo imefanyika mkoani Mtwara, ambapo maafisa wa TANROADS walifika katika shule mbalimbali na vituo vya bodaboda kutoa mafunzo ya kinadharia na vitendo. Wanafunzi walielimishwa namna ya kuvuka barabara kwa usalama na kuzingatia sheria za usalama, wakizingatiwa kama miongoni mwa makundi yaliyo hatarini kuathirika na ajali. “Kuwafikia wanafunzi kutawasaidia kujenga uelewa wa mapema kuhusu kanuni za usalama barabarani na kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika,” walibainisha maafisa hao.

Kwa upande wa waendesha bodaboda, TANROADS ilisisitiza uvaaji wa kofia ngumu (helmet), kufuata sheria za usalama barabarani na kuepuka mwendo holela hususan karibu na shule na maeneo yenye mkusanyiko wa watu. Vilevile, pikipiki zao zilikaguliwa ili kuhakikisha zipo katika hali nzuri ya kiusalama.

Katika mafunzo hayo, wanafunzi walipata nafasi ya kuuliza maswali, pamoja na kupewa vifaa vya usalama ikiwemo reflector na vipeperushi vyenye maelekezo ya usalama barabarani.

TANROADS imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha usalama barabarani nchini, hususan kwa makundi yenye uhitaji maalum kama wanafunzi na waendesha bodaboda, sambamba na watumiaji wengine wa barabara.