WATUMIAJI WA BARABARA YA CHAMWINO – DABALO – ITISO WAPATA SULUHISHO LA KUDUMU LA DARAJA
Dodoma
20/8/2025
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, ametembelea mradi wa ujenzi wa daraja jipya lenye urefu wa mita 60 na upana wa mita 11.6 katika eneo la Nzali – Chilono, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Daraja hili litakuwa na njia pana za magari na maeneo ya watembea kwa miguu ili kuongeza usalama na ufanisi wa usafiri.
Ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hili ni sehemu ya miradi ya dharura iliyoanzishwa kufuatia madhara ya mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha kuanzia Novemba 2023 hadi Mei 2024 na kuathiri maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma. “Daraja la Nzali – Chilono lilikuwa dogo na mara nyingi lilisababisha mafuriko, hivyo kuathiri usafiri na maisha ya wananchi. Hii barabara ya Chamwino – Dabalo – Itiso ni muhimu sana, ndiyo maana Serikali imeona umuhimu wa mradi huu,” alisema Mhandisi Zuhura.
Kwa sasa, kazi za ujenzi zinaendelea chini ya mkandarasi CHICO kutoka China kwa gharama ya shilingi bilioni 14.5, chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri kutoka TANROADS (TECU). Hadi sasa, nguzo 36 zimekwishachimbiwa, kalavati na kingo za daraja zimekamilika, na kazi ya kujaza kifusi katika maingilio ya daraja inaendelea.
Mradi huu ulianza rasmi tarehe 15 Novemba 2024 na ulipangwa kukamilika ifikapo 14 Novemba 2026. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wake, mkandarasi ameongeza kasi ya kazi kwa kufanya kazi hadi muda wa ziada ili ukamilike kabla ya msimu wa mvua. “Hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 62.8 na matarajio yetu ni kumaliza mradi huu mapema mwezi Oktoba 2025,” alisisitiza Mhandisi Zuhura.
Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hili umezingatia viwango vyote vya kitaalamu na umeandaliwa kuendana na uboreshaji wa baadaye wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami bila kubomoa daraja. Pia daraja litafungwa taa maalum kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wasafiri na wasafirishaji.
Mhandisi Zuhura alibainisha kuwa kukamilika kwa daraja hili kutarahisisha shughuli za kila siku ikiwemo usafirishaji wa mazao ya kilimo, huduma za biashara na usafiri wa abiria, hivyo kuchochea uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.
Aidha, aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha na kuona umuhimu wa mradi huu.
Kwa upande wake, Mhandisi Sun Pelxin kutoka kampuni ya CHICO alisema mradi huu ulipangwa kuisha Novemba 2025, lakini kutokana na kasi nzuri ya utekelezaji, wanatarajia kuukamilisha mwishoni mwa mwezi Oktoba 2025.