SERIKALI KUTUMIA BILIONI 45 KWA UJENZI WA MIRADI YA DHARURA MKOANI KAGERA
Kagera
21 Agosti, 2025
Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 45 kwaajili ya ujenzi wa madaraja Matano ambayo yamekuwa kero kubwa wakati wa msimu wa mvua kupelekea kusimama kwa shughuli za uzalishaji mkoani Kagera.
Akitoa ufafanuzi wa maendeleo ya miradi hiyo Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera Mhandisi Ntuli Mwaikokyesa amesema, miradi hiyo imefikia hatua tofauti za utekelezaji na wakandarasi wanatarajia kuikamilika kwa wakati kwa mujibu wa mikataba.
Mha. Ntuli ameongeza kuwa daraja la Kanoni linalojengwa na mkandarasi Abemulo Consultant lililopo katikati ya mji lenye urefu wa mita 30 na barabara za maungio mita 600 zimefikia asilimia 50 za utekelezaji na kukamilika kwake kutarahisisha usafiri na usafishaji.
Kwa upande wake Mha. Aloyce Kamala, ambaye ni mwakilishi wa Mkandarasi amesema mradi huo utakamilika kwa wakati kutokana na kazi kufanyika usiku na mchana, huku akieleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutaondoa kero ya mafuriko katika eneo hilo.
Sambamba na ujenzi wa daraja la Kanoni, Mkandarasi huyo anatekeleza mradi wa barabara ya njia nne, ambao hadi sasa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji na una gharimu kiasi cha billioni 5.