BILIONI 26.15 ZAONDOA KERO YA MAFURIKO ENEO LA MTANANA - DODOMA
Dodoma
20 Agosti, 2025
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wameweza kuondoa kero ya mafuriko ya mara kwa mara ya maji yanayotokana na mvua katika eneo la Mtanana mkoani Dodoma kwa kunyanyua tuta la barabara wenye urefu wa kilometa sita ambao umegharimu Bilioni 26.15
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani amesema kuwa eneo hilo lilikuwa na kero kubwa wakati wa mvua za El-Nino kutokana na maji mengi kutoka milimani kupita juu ya daraja na pia juu ya barabara na kusababisha mafuriko yaliyowafanya watumiaji wa barabara hiyo kushindwa kupita kwa saa kadhaa.
Mhandisi Zuhura amesema mbali na kunyanyuliwa kwa tuta hilo, pia wamejenga makalavati makubwa saba yenye ukubwa tofauti, yatakayoweza kupitisha maji kwa wingi kwa wakati mmoja, tofauti na awali yaliyokuwapo yalizidiwa na uwingi wa maji.
Amesema anaishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya mradi huu ambao unasimamiwa na TANROADS mkoa wa Dodoma, na unatekelezwa na Mkandarasi Mzawa, kampuni ya Estim Construction.
“Utekelezaji wa mradi huu ulianza tarehe 13 Juni, 2024 na kwa mujibu wa mkataba ambapo unatarajiwa kukamilika tarehe 13 Novemba, 2025, na kama mnavyoona barabara hii kuu ni muhimu Mkandarasi amefanya kazi kwa juhudi ikiwemo kufanya kazi zaidi ya muda,” amesema Mhandisi Zuhura.
Mhandisi Zuhura amesema tayari Mkandarasi amekamisha kazi mbalimbali zikiwemo ujenzi wa madaraja yote saba, kuinua tuta, kuweka matabaka mbalimbali ya kifusi na uwekaji wa lami.
Hatahivyo, amesema TANROADS mkoa Dodoma wanaendelea kusimamia kwa karibu ujenzi huu ili Mkandarasi aweze kujenga kwa viwango vilivyowekwa na hadi sasa utekelezaji wa mradi huu hadi sasa umefikia asilimia 97.
Vilevile, Mkandarasi anatarajia kukamilisha uwekaji wa alama za barabarani na baadaye ataweka taa kwa ajili ya usalama wa wanaopita kwenye barabara hiyo pamoja na miundombinu iliyopo.