WANANCHI WAMSHUKURU RAIS DKT. SAMIA KWA UJENZI WA BARABARA YA KAHAMA-KAKOLA
Kahama
18/08/2025
Wananchi wa Kata ya Ntobo, Halmashauri ya Msalala, wamempongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutekeleza ujenzi wa barabara ya Kahama–Kakola yenye urefu wa kilomita 73, ambayo inatarajiwa kuondoa kero ya muda mrefu ya usafiri katika eneo hilo.
Mtendaji wa Kata ya Ntobo, Bi Aisha Mabute, amesema wananchi wanashuhudia kasi kubwa ya utekelezaji kwani wakandarasi wanafanya kazi mchana na usiku bila kusita, akisisitiza kuwa “juhudi tunaziona kwa macho; kazi inaendelea asubuhi, mchana na usiku.”Wananchi kwa ujumla wamesema walikuwa wakikumbana na changamoto ya kusafirisha mazao na huduma za dharura, na wameipongeza Serikali kwa jitihada madhubuti za kuboresha miundombinu.
Wamebainisha kuwa barabara hiyo itarahisisha usafiri na usafirishaji, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.