TANROADS Kujenga Barabara ya Njia Nne na Mwendokasi Kufungua Uchumi wa Mwanza
Mwanza,
04 Aug, 2025
Serikali ya Tanzania imejipanga kikamilifu kuleta mapinduzi ya miundombinu katika Jiji la Mwanza kupitia ujenzi wa barabara ya njia nne yenye njia ya mwendokasi, hatua inayolenga kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa jiji hilo na mikoa jirani.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal alisema kuwa maandalizi ya ujenzi yamekamilika na utekelezaji utaanza mara tu baada ya kumpata mkandarasi mshindi wa zabuni iliyotangazwa.
“Barabara hii itakuwa ya njia nne na katikati yake tutaweka njia ya mwendokasi kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Hii ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kupunguza msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Mwanza Mjini hadi Usagara,” alisema Mhandisi Pascal.
Aidha, Mhandisi Pascal alibainisha kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Serikali Kuu inaendelea kugharamia miradi mingine muhimu ya barabara, ikiwemo ujenzi wa daraja la Simiyu lililopo umbali wa kilomita 65 kutoka Mwanza mjini na kilomita 3 kutoka Magu. Daraja hilo linatekelezwa na kampuni ya CCECC kwa gharama ya Shilingi bilioni 48, ambapo hadi sasa limekamilika kwa asilimia 60 na linatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 30, 2025.
Kwa mujibu wa Mhandisi Pascal, daraja la Simiyu lina urefu wa kilomita 1.75 na litaambatana na ujenzi wa barabara unganishi ya kilomita 3. Kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha sana usafiri kwa kuwa kwa sasa magari yanapita kwa zamu upande mmoja, hali inayosababisha msongamano mkubwa.
Katika hatua nyingine, TANROADS inaendelea na ujenzi wa daraja la Sukuma, linalotekelezwa na mkandarasi mzawa, Mumangi Construction Co. Ltd kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.78. Daraja hilo hadi sasa limefikia asilimia 60 ya utekelezaji na litaambatana na ujenzi wa barabara unganishi ya kilomita 2.3, ambapo mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2025.
Mhandisi Pascal alisema kuwa miradi hiyo mikubwa ya uboreshaji wa miundombinu italeta tija kubwa kwa uchumi wa wakazi wa Mwanza na maeneo jirani. “Uboreshaji huu utapunguza muda wa safari na kupunguza gharama za usafirishaji wa watu na bidhaa, hivyo kuinua shughuli za kibiashara,” alieleza.
Alitoa mfano wa daraja la Sukuma lililopo Magu, akisema litawarahisishia wasafiri wanaotoka Bariadi kupitia Mahaha kwa kutumia barabara ya Magu – Mahaha, ambayo ni fupi kwa takriban kilomita 40 ikilinganishwa na njia ya Lamadi.
Zaidi ya hayo, Mhandisi Pascal alisema kuwa upembuzi yakinifu unaendelea kufanyika kwa ajili ya kuipandisha hadhi barabara hiyo hadi kiwango cha lami. Kazi hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Kampuni ya Saba kutoka Ethiopia na wataalamu wazawa.
“Baada ya upembuzi kukamilika na barabara kuwekwa lami, tunaamini barabara hii itakuwa chaguo bora kwa wasafiri kutoka Magu kwenda Bariadi na maeneo ya jirani,” alihitimisha.