BARABARA YA LUSAHUNGA–RUSUMO (KM 92) KUONDOA KERO YA USAFIRI NA KUCHOCHEA MAENDELEO KANDA YA ZIWA
Kagera
29/07/2026
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuboresha kwa kiwango cha lami barabara ya Lusahunga–Rusumo yenye urefu wa kilometa 92, iliyopo mkoani Kagera. Barabara hii ni kiungo muhimu kwa usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na imekuwa na changamoto kubwa kutokana na msongamano wa magari makubwa ya mizigo.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi George Mwandike alieleza kuwa ujenzi huo unagharimu shilingi bilioni 153 na unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) chini ya usimamizi wa washauri elekezi kutoka kampuni ya NORPLAN Tanzania kwa kushirikiana na TYPSA ya Hispania. Hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari 2026 kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.
Mhandisi Mwandike aliongeza kuwa pamoja na kuboresha barabara kuu kwa kiwango cha lami, mradi huo utahusisha pia ujenzi wa barabara za waenda kwa miguu zenye urefu wa kilometa 12 katika maeneo ya miji inayopitiwa na barabara hiyo. Vilevile, taa za barabarani zitafungwa ili kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara hasa nyakati za usiku.
“Mbali na barabara, tumepanga pia kugusa jamii kwa kujenga shule na kuboresha zahanati kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5,” alisema Mwandike.
Aidha, alitoa shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo ambayo itarahisisha usafiri, kukuza biashara za mipakani, na kuongeza mapato ya taifa kupitia uboreshaji wa miundombinu ya kiuchumi.
Barabara ya Lusahunga–Rusumo inatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Kagera na wakazi wa nchi jirani wanaotegemea Tanzania kwa shughuli zao za usafirishaji na biashara.