GEITA YAPATA SULUHISHO LA KUDUMU KWA MIUNDOMBINU YA BARABARA
Geita
27/7/2025
Mkoa wa Geita ulikuwa miongoni mwa maeneo yaliyokumbwa na athari kubwa za mvua za El Niño, zilizoharibu miundombinu muhimu ya barabara kuu na barabara za mkoa. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imechukua hatua madhubuti kwa kujenga madaraja makubwa na barabara za maungio (approach roads) katika eneo la Masumbwe–Mwabomba.
Akizungumza kuhusu juhudi hizo, Mhandisi Fredrick Mande alieleza kuwa serikali imetekeleza ujenzi upya wa miundombinu katika maeneo yaliyoharibiwa vibaya na mvua, ikiwemo eneo la Wendele–Mlele. Hatua hii inalenga kuondoa kabisa kero ya usafiri na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa urahisi kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mande, kazi hiyo inajumuisha ujenzi wa tuta unganishi lenye urefu wa jumla ya kilomita 1.5, ujenzi wa makalavati makubwa saba, pamoja na tabaka la juu la barabara.
"Mkandarasi anaendelea na kazi mchana na usiku ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kama masharti ya mkataba yanavyoelekeza," alisisitiza Mande.
Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, hata katika maeneo yaliyoathirika na majanga ya asili, kwa lengo la kukuza uchumi wa wananchi na kuimarisha maendeleo ya taifa kwa ujumla.