TANROADS Dodoma Yawahamasisha Wajenzi Wapime Malighafi kwa Gharama Nafuu Kupitia Maabara Yake ya Kisasa
26/07/2025
Bahati Mollel - Dodoma
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia maabara yake ya mkoa wa Dodoma, imewahimiza wakandarasi, taasisi za serikali na wajenzi binafsi kutumia huduma za upimaji wa malighafi kwa gharama nafuu kabla ya kuanza au kuendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu.
Wito huo umetolewa na Msimamizi wa Vifaa na Vipimo wa Maabara hiyo, Mhandisi Faustine Makumbi, ambaye amesema kuwa maabara hiyo hutoa huduma za kitaalamu za upimaji wa ubora wa malighafi zinazotumika kwenye ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu mingine muhimu.
“Tunaweza kusaidia wajenzi kubaini kama malighafi zao zinakidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuanza matumizi, jambo ambalo linaepusha hasara na husaidia kujenga miundombinu imara na ya kudumu,” amesema Mhandisi Makumbi.
Amefafanua kuwa maabara hiyo inafanya upimaji kwa njia mbalimbali, ikiwemo kutumia mashine maalum ya nyuklia (Troxler) kupima kiwango cha mgandamizo moja kwa moja eneo la kazi, pamoja na kutumia mbinu ya "sand replacement" inayohusisha uchukuaji wa sampuli ya mchanga au udongo kwa ajili ya uchunguzi wa kina maabara.
Kwa upande wake, Fundi Sanifu Msaidizi wa Maabara, Bw. Adolf Ngawambara, amesema maabara hiyo ina uwezo mkubwa wa kupima lami kwa kutumia teknolojia ya kisasa. “Tunatumia petroli kutenganisha lami na kokoto, kisha tunakausha kokoto hizo kwa saa tatu hadi nne ili kupata taarifa sahihi za ubora wake,” ameeleza.
Aidha, Mhandisi Msaidizi wa Maabara, Bw. Joel Sanga, amesema maabara hiyo pia hupima uimara wa kokoto dhidi ya mshtuko na mkandamizo. “Kokoto hukatwa kwa milimita 10, hupimwa kwa mashine maalum, na kupatikana vipimo sahihi vya uimara unaohitajika kwenye ujenzi bora,” amesema.
Bi. Stella Chedego, Fundi Sanifu anayehusika na vipimo vya udongo, amesema wao hupima tabia za udongo kwa kuuhifadhi kwa saa 24 ili kugundua viambato kama maji na plastiki vilivyomo. “Matokeo haya ni muhimu sana katika kutambua utendaji wa udongo mahususi kabla ya kuanza ujenzi,” amesema.
Naye Bw. Kaja Kisiwa, Fundi Sanifu Msaidizi, amesema wanafanya majaribio ya mshindilio wa barabara baada ya hatua za awali za usawazishaji ili kuhakikisha uimara na uthabiti wa barabara inayojengwa.
Akihitimisha, Mhandisi wa Maabara, Bi. Getrude Enock ametoa mwito wa wazi kwa wajenzi wote—wanaoshirikiana na TANROADS na wale wa sekta binafsi—kutumia huduma za maabara hiyo.
“Tunakaribisha wajenzi wote kuja kupima malighafi zao hapa. Tuna vifaa vya kisasa, matokeo ya haraka na gharama zetu ni nafuu. Kupima ni hatua muhimu ya kuhakikisha miundombinu tunayojenga ni salama, bora na ya kudumu, kwa maendeleo ya taifa,” amesema Bi. Getrude.
Kwa maelezo zaidi kuhusu huduma za maabara ya TANROADS Dodoma, tafadhali wasiliana na ofisi ya mkoa.