Dar es salaam
16/07/2025
MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA: DAR ES SALAAM YAVUNA MATUNDA YA UWEKEZAJI WA MIUNDOMBINU.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jiji la Dar es Salaam limeendelea kung’ara kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu iliyobadilisha sura ya jiji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiusalama.
Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Ananuswe Kyamba, jiji lina mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 619.01, ambapo sehemu kubwa ni njia za upana wa njia nne hadi nane. Mtandao huu umeongeza ufanisi katika usafirishaji na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Mhandisi Kyamba anabainisha kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, TANROADS mkoani humo imekamilisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa madaraja ya juu ya Chang’ombe, Uhasibu, Gerezani pamoja na Daraja la Tanzanite linalounganisha Posta na Masaki – yote yakiwa ni mafanikio yanayolifanya jiji kuwa la kisasa zaidi.
“Tumeshuhudia maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia. Tumejenga na kukamilisha madaraja ya juu pamoja na barabara za BRT Awamu ya Pili, na sasa tunakaribia kukamilisha BRT Awamu ya Tatu,” alisema Kyamba.
Mradi wa BRT Awamu ya Pili unaoanzia katikati ya jiji hadi Mbagala tayari umekamilika na unatarajiwa kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Temeke na maeneo ya kusini. Wakati huo huo, utekelezaji wa BRT Awamu ya Tatu, unaohusisha barabara nyingine muhimu za jiji, uko katika hatua za mwisho.
Katika kukabiliana na changamoto ya msongamano, Serikali imepanua barabara ya kutoka Ubungo hadi Kimara kutoka njia nne hadi sita. Kazi hiyo, ambayo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 50, inatarajiwa kuhitimishwa ifikapo Septemba mwaka huu.
“Msongamano katika barabara ya Kimara–Ubungo ulikuwa kero kubwa, ndipo Mheshimiwa Rais akaelekeza upanuzi wa sehemu hiyo ili kurahisisha na kuharakisha safari za wakazi,” alifafanua Mhandisi Kyamba.
Katika eneo la taa za barabarani, zaidi ya taa 972 zimefungwa katika kipindi cha miaka minne, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufanya Dar es Salaam kuwa jiji linalofanya kazi saa 24. “Kwa sasa, Kariakoo nzima inang'aa. Tuna jumla ya taa 2,800, ambapo 972 zimefungwa ndani ya kipindi cha miaka minne,” alisema.
Mradi mwingine unaoendelea ni wa BRT Awamu ya Nne unaotoka Posta na kupita maeneo mengine ya jiji, kwa lengo la kuimarisha zaidi mfumo wa usafiri wa haraka na kupunguza msongamano wa magari.
Kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imetumia zaidi ya shilingi trilioni 1.6 katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya miradi ya miundombinu, ikijumuisha ujenzi wa barabara, madaraja, taa na maboresho ya mfumo wa usafiri wa umma.
“Tunampongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa maono yake makubwa ya kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji la kisasa lenye miundombinu ya kuaminika inayochochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” alihitimisha Mhandisi Kyamba.