News

MWENGE WA UHURU WATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA DARAJA LA BOX CULVERT MSASANI-MANYARA

Manyara

16/07/2025

MWENGE WA UHURU WATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA DARAJA LA BOX CULVERT MSASANI, MANYARA.

Mwenge wa Uhuru umefika katika eneo la Msasani, Wilaya ya Babati, kutembelea mradi wa ujenzi wa daraja la Box Culvert linalotekelezwa na TANROADS Mkoa wa Manyara. Ugeni huo ulipokelewa na Meneja wa TANROADS mkoani humo, Mhandisi Dutu Masele, pamoja na timu ya wahandisi walioko katika eneo la mradi.

Katika tukio hilo, viongozi mbalimbali wa serikali walikuwepo, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Kaganda, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mjini. Wananchi wa Msasani nao walijitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo muhimu.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 alielezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya mradi huo na kupongeza TANROADS kwa usimamizi madhubuti wa kazi. “Mradi huu ni wa muhimu kwa jamii. Utekelezaji wake utapunguza kwa kiasi kikubwa kero za usafiri na kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara,” alisema.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara, Mhandisi Dutu Masele, alieleza kuwa ujenzi wa daraja hilo ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto zilizokuwa zikilikabili eneo hilo. “Kupitia mradi huu, wananchi wa Msasani wataondokana na adha kubwa waliyokuwa wakikumbana nayo hasa wakati wa mvua,” alisema Mhandisi Masele.

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha miundombinu ya barabara nchini, kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi vijijini na mijini.