News

MKUU WA MKOA WA SONGWE MHE. JABIRI MAKAME ATEMBELEA KITUO CHA MIZANI MPEMBA

Songwe

14/07/2025

 

MKUU WA MKOA WA SONGWE MHE. JABIRI MAKAME ATEMBELEA KITUO CHA MIZANI MPEMBA

Leo tarehe 14 Julai 2025, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Jabiri Omari Makame amefanya ziara ya ukaguzi katika Kituo cha Mizani cha Mpemba, kilichopo barabara kuu ya kuelekea Tunduma, mkoani Songwe.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufuatilia kwa karibu namna shughuli za upimaji wa magari zinavyoendeshwa, na kuona hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo muhimu la usafirishaji. Eneo la Tunduma/Mpemba linapokea zaidi ya asilimia 72 ya magari yote yanayopita kutoka Tanzania kwenda nchi za SADC na DRC Congo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, amemueleza Mhe. Makame kuwa kituo hicho kinatumia mfumo wa kidigitali kuhifadhi taarifa za magari yanayopimwa. Ameongeza kuwa kutokana na ongezeko la magari, Serikali imeongeza mizani ya mkeka (mobile weighbridge), hatua ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari.

Pia, Mhandisi Bishanga amebainisha kuwa Serikali kupitia TANROADS iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya ujenzi wa mizani kubwa katika eneo la Iboya pamoja na upanuzi wa barabara kutoka Tunduma hadi Igawa, ili kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo.

Kwa niaba ya TANROADS, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia utoaji wa fedha za kuboresha barabara zenye changamoto ndani ya Mkoa wa Songwe, hususan maeneo ya Mpemba – Tunduma na Senjele II. Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuanza muda mfupi ujao.

Hatua hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza usumbufu kwa wasafirishaji na kuimarisha huduma za uchukuzi barabarani katika njia hii ya kimkakati.

#SongweYajengwa

#TANROADS

#MiundombinuBora

#SamiaKazini

#WeighbridgeMpemba

#SADCTransport