News

DKT TAX AITAKA TANROADS KUKAMILISHA BARABARA KUELEKEA MAKAO MAKUU YA TPDF

DKT. STERGOMENA TAX

Dodoma

10/07/2025

DKT. TAX AITAKA TANROADS KUKAMILISHA BARABARA KUELEKEA MAKAO MAKUU YA TPDF

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax, ametoa wito kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuongeza kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Kikombo–Chilolo–Mapinduzi inayounganisha na Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF), mkoani Dodoma.

Akizungumza tarehe 10 Julai 2025 wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Dkt. Tax alisisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu mkandarasi ili kuhakikisha kazi inasonga kwa haraka na kwa viwango vinavyotakiwa.

“Niwaombe muongeze bidii ili muweze kukamilisha  ujenzi i,” alihimiza.

Aidha, Waziri huyo alisisitiza kuwa na mpango kazi wa kila wiki unaoainisha hatua kwa hatua shughuli za utekelezaji ili kuharakisha ukamilishaji wa barabara hiyo muhimu kwa shughuli za kiulinzi na kijamii.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, alieleza kuwa tayari michoro ya madaraja manne imepitishwa na kuidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji. Aliongeza kuwa katika sehemu ya barabara inayopita ndani ya eneo la jeshi yenye urefu wa kilomita 4.2, kazi ya ujazaji wa udongo inaendelea sambamba na ukarabati wa barabara ya mchepuo (diversion road) ambayo ipo katika hatua ya kuimarishwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya miundombinu yenye tija kwa wananchi.

“Barabara hii inagusa maisha ya wananchi na itawarahisishia kupata huduma mbalimbali za kijamii,” alisema Mhe. Mayanja.

Ujenzi wa barabara ya Kikombo–Chilolo–Mapinduzi ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiulinzi kupitia uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya barabara.