MHANDISI ALOYCE MATEI
Dar es salaam
SERIKALI KUPITIA TANROADS YAZINDUA MWONGOZO MPYA WA UJENZI WA BARABARA KUIMARISHA UBORA NA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATENGENEZO
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) leo Ijumaa Julai 04, 2025 imezindua rasmi Mwongozo wa Uhakiki na Udhibiti wa Ubora wa Kazi za Ujenzi wa Barabara za Lami (Guidelines for Quality Assurance and Quality Control of Bituminous Road Works), ikiwa ni hatua mahsusi ya kuboresha viwango vya ubora wa barabara na kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo, Mhandisi Aloyce Matei amesema mwongozo huo unaweka msingi wa kuhakikisha kazi za ujenzi wa barabara, hasa zile za lami, zinazingatia viwango stahiki vya kitaalamu kwa lengo la kudumu zaidi na kuleta tija kwa taifa.
"Mwongozo huu ni miongoni mwa mikakati mahsusi ya serikali ya kukabiliana na changamoto zinazohusiana na ubora wa kazi za ujenzi wa barabara. Serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta hii muhimu, ikiwemo mipango ya muda mrefu na kuanzisha taasisi kama TANROADS kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya barabara nchini," alisema Mhandisi Matei.
Amesema tangu mwaka 1990, serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya uendelezaji na ukarabati wa barabara, ikiwa ni pamoja na kuhuisha barabara za changarawe kuwa za lami, kukarabati barabara zilizochakaa, kuboresha barabara za vijijini kuelekea mashamba, na kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kusimamia miradi hiyo.
Kwa sasa, mtandao wa barabara kuu nchini una jumla ya kilomita 37,435, ambapo kati ya hizo, kilomita 12,203 ni za lami na kilomita 25,232 ni za changarawe.
Tangu kuanzishwa kwa TANROADS miaka ya 2000, mtandao wa barabara za lami umeongezeka kutoka kilomita 3,800 hadi 12,203. Ongezeko hili limetokana na juhudi za serikali za kuboresha sekta ya usafirishaji kwa lengo la kukuza uchumi wa wananchi.
"Hata hivyo, kutokana na ongezeko la magari mazito, mabadiliko ya tabianchi, na maendeleo ya kiuchumi, barabara nyingi zimekuwa zikiharibika mapema kabla ya muda wake wa matumizi kuisha. Hali hii imesababisha serikali kuingia gharama kubwa za matengenezo na hivyo tukaona ni muhimu kuandaa mwongozo huu," alieleza.
Mhandisi Matei amebainisha kuwa Wizara kupitia TANROADS ilianza utafiti mwaka 2016 na mwaka 2018 ikaandaa mwongozo wa mchanganyiko wa zege la lami unaohimili hali halisi ya Tanzania.
Kazi ya kuhuisha miongozo mingine inaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema mwongozo huu mpya umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya TANROADS na Chuo Kikuu cha Pretoria cha Afrika Kusini kupitia tafiti mbalimbali.
Mhandisi Besta amesema, mafunzo ya miezi minne yalitolewa kwa wahandisi wa TANROADS kuhusu masuala ya udhibiti wa ubora kabla ya kuandaa mwongozo huo.
"Tunatoa ahadi kama TANROADS ya kuendelea kuwa waaminifu katika kuhakikisha tunatekeleza miradi ya barabara kwa ubora wa hali ya juu. Kaulimbiu yetu ya 'Barabara Bora kwa Maendeleo ya Taifa' itaendelea kutuongoza," alisema Mhandisi Besta.
Mwongozo huu umezingatia pia teknolojia za kisasa, uhalisia wa mazingira ya Tanzania, na unalenga kuhakikisha thamani ya fedha inayotumika katika miradi ya ujenzi wa barabara inaonekana. Aidha, mwongozo huu umetayarishwa kwa ushirikiano na Baraza la Utafiti la Afrika Kusini (CSIR) na wadau mbalimbali wakiwemo wakandarasi, wahandisi washauri, na wataalamu wa sekta ya ujenzi.
Wito umetolewa kwa taasisi za elimu ya juu kuutumia mwongozo huu kama nyenzo ya kuandaa wataalamu wa siku zijazo katika sekta ya ujenzi wa barabara.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Utafiti la Afrika Kusini (CSIR) Bi. Nomsa Dlamini ameeleza kufurahishwa kwake na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi yake na TANROADS katika maandalizi ya mwongozo huo. Alisema, “Napenda kuishukuru TANROADS kwa ushirikiano wao wa dhati katika mradi huu wa kuandaa mwongozo wa udhibiti na uhakiki wa ubora wa kazi za ujenzi wa barabara. Ushirikiano huu unaendelea kuimarika na tunaamini utaendelea kuzaa matunda kwa manufaa ya pande zote mbili.”
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesisitiza kuwa utekelezaji wa mwongozo huu utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha uharibifu wa mapema wa barabara na kuongeza ufanisi wa kazi zinazofanywa kwa gharama za umma.