MH. MOHAMED BESTA-MTENDAJI MKUU TANROADS
Dar es salaam
05/07/2025
MTENDAJI MKUU TANROADS: MWONGOZO WA UDHIBITI WA UHAKIKI WA UBORA WA KAZI ZA UJENZI WA BARABARA UMEKIDHI VIWANGO VYA UBORA VYA KIMATAIFA
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha ubora wa miundombinu nchini kwa kuzindua Mwongozo mpya wa Udhibiti na Uhakiki wa Ubora wa Kazi za Ujenzi wa Barabara, ambao umetajwa kuwa umekidhi viwango vya ubora vya kimataifa.
Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema mwongozo huo ni matokeo ya uchambuzi wa kina uliofanywa na TANROADS kwa lengo la kukabiliana na changamoto za ujenzi usiofikia viwango na kuimarisha usimamizi wa miradi ya barabara.
"Utekelezaji wa mapendekezo ya uchunguzi wa awali upo katika hatua nzuri ikiwa ni pamoja na uandaaji wa mwongozo huu wa Guidelines for Quality Assurance and Quality Control of Bituminous Road Works," alisema Mhandisi Besta.
Amesema mwongozo huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Pretoria cha Afrika Kusini, na umezingatia matumizi ya teknolojia za kisasa katika udhibiti wa ubora, ikiwa ni pamoja na taratibu za kupata mchanganyiko bora wa lami (asphalt concrete).
Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, lengo kuu la mwongozo huu ni kuhakikisha uwepo wa uwiano wa kitaifa katika usimamizi wa ubora wa ujenzi wa barabara, kuondoa mianya ya makosa, kuongeza ubora wa kazi na kupunguza gharama za matengenezo.
Amefafanua kuwa miongozo ya namna hii imekuwa ikiandaliwa na serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali tangu mwaka 1974, ambapo toleo la kwanza la "Yellow Book" lilianzishwa kwa msaada wa Transport Research Laboratory ya Uingereza.
Miongozo hiyo imekuwa ikiboreshwa mara kwa mara, ikihusisha pia ushiriki wa Norway Public Road Administration, pamoja na wataalamu wa ndani.
“TANROADS iko kwenye mchakato endelevu wa kuhuisha na kuandaa miongozo mipya, kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya usafiri na barabara,” alisema.
Ameongeza kuwa kabla ya uzinduzi wa mwongozo huo, wahandisi wa TANROADS walipatiwa mafunzo ya miezi minne kuhusu usimamizi wa ubora katika ujenzi wa barabara, ikijumuisha kazi za lami, changarawe, zege na malighafi nyingine.
Kupitia Kitengo chake cha Utafiti, TANROADS itaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo kupitia semina, warsha na wavuti, ili kuhakikisha matumizi sahihi ya mwongozo huo kwenye miradi ya barabara nchini.
Aidha, Mhandisi Besta amesema TANROADS itaongeza ushirikiano na kurugenzi za ndani pamoja na taasisi ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha miongozo hiyo inajumuishwa kwenye nyaraka rasmi za usimamizi wa miradi, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na viwango stahiki.