“MIAKA MICHACHE IJAYO TANZANIA KUJITEGEMEAKIKAMILIFU UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU” - ULEGA
Dar es Salaam
22 Juni, 2025
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya ujenzi nchini ni matokeo ya maono, juhudi, ubunifu na rasilimali za Watanzania wenyewe.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza katika hafla ya Jukwaa la Fikra iliyofanyika tarehe 22 Juni 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Ulega amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya madaraja manane yamekamilika kujengwa huku madaraja mengine 12 yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.
“Mheshimiwa Rais ameweka bayana kuwa ujenzi wote tulioufanya kwa kipindi hiki ni matokeo ya maono yetu na jasho letu wenyewe. Haya ni mafanikio ya Watanzania, hivyo tujipongeze kwa kazi nzuri,” alisema Waziri Ulega.
Waziri Ulega amebainisha kuwa sekta ya ujenzi ina matarajio makubwa ya kuendelea kujenga barabara nyingi na madaraja zaidi, lakini pia kuna mahitaji mengine muhimu kwa taifa yanayohitaji kutekelezwa kwa hatua.Katika mkutano huo, Waziri Ulega ameeleza kuwa serikali imeanza kutoa kandarasi kwa kampuni za wazawa, zikiwemo kampuni za wanawake.
“Hivi karibuni tumewapa kandarasi zaidi ya kampuni nane zinazoongozwa na kinamama katika miradi mbalimbali hususan mkoa wa Songwe,” aliongeza.Pia ametaja mafanikio ya wazawa katika sekta ya usanifu na usimamizi wa miradi mikubwa ya ujenzi, akitoa mfano wa Mhandisi Katelula Kaswaga, kijana wa miaka 35, ambaye ndiye msimamizi wa daraja la J.P Magufuli na daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525, pamoja na daraja la Simiyu.
“Faida mojawapo ya miradi hii ni kuwaandaa na kuwajenga wataalamu wetu wa ndani na kuwa wabobezi. Katika miaka michache ijayo, Tanzania itakuwa na uwezo wa kujitegemea kikamilifu kwenye miradi ya ujenzi,” alieleza Ulega na kuongeza "Tanzania itakuwa na uwezo, na haitakuwa na haja ya kuchukua mtu yeyote kutoka mahali popote. Tutafanya wenyewe kwa fedha, ubunifu na mazingira yetu wenyewe" Jukwaa hilo limeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, likiongozwa na kauli mbiu “Kujenga Madaraja, Kujenga Taifa: Miundombinu Kichocheo cha Ukuaji Jumuishi.”