SERIKALI YASAINI MIKATABA YA UJENZI WA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI MKOANI SONGWE
22 Juni, 2025
Songwe
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesaini mikataba miwili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika mkoa wa Songwe, hatua inayolenga kuboresha miundombinu, kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Mikataba hiyo imesainiwa mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, katika hafla iliyofanyika Juni 22, 2025 mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi wa mkoa, wilaya, wabunge, na wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo muhimu.
Katika mikataba hiyo, TANROADS iliwakilishwa na Mtendaji Mkuu wake, Mha. Mohamed Besta, aliyeweka saini kwa niaba ya Serikali, pamoja na wahandisi wakuu wa miradi hiyo.
Miradi iliyosainiwa ni pamoja na ujenzi wa sehemu ya barabara ya kimkakati ya Kamsamba–Mlowo, ambapo kilomita 10 zitajengwa katika awamu ya pili — kilomita tano kutoka Kamsamba kuelekea Kankoko na kilomita tano kutoka Mlowo kuelekea Kamsamba.
Pia, Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mkwajuni–Patamera–Makongorosi, ambayo inalenga kuunganisha maeneo ya uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, hasa katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Daniel Chongolo, alisema miradi hiyo si ya kimkoa pekee bali ni ya kimkakati kwa taifa zima.“Barabara hizi si za mkoa wa Songwe pekee, bali ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya kitaifa. Barabara ya Kamsamba–Mlowo imeunganisha wilaya mbili — Momba na Mbozi — na mikoa miwili — Rukwa na Songwe.
Hii ni njia kuu ya mkato kutoka Rukwa kwenda mikoa ya kusini na kati ya Tanzania,” alisema Chongolo na kuongeza “…Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutekeleza maendeleo kwa vitendo.”
Wananchi waliopata nafasi ya kuzungumza walieleza furaha yao kutokana na hatua hiyo ya Serikali.
Walisema barabara hiyo ni muhimu kwa usafirishaji wa mazao kama mpunga na ufuta katika Wilaya ya Momba na maeneo ya jirani, na waliiomba Serikali kuhakikisha kasi ya utekelezaji haikatizwi.