News

MTENDAJI MKUU TANROADS AFANYA UKAGUZI WA MIUNDOMBINU KATIKA MIKOA YA KATAVI, RUKWA NA SONGWE

MTENDAJI MKUU TANROADS AFANYA UKAGUZI WA MIUNDOMBINU KATIKA MIKOA YA KATAVI, RUKWA NA SONGWE

22 Juni, 2025

Songwe

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amefanya ziara ya ukaguzi wa barabara na madaraja katika mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Ukanda wa Magharibi na Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania.

Ziara hiyo imelenga kufuatilia maendeleo ya miundombinu ya barabara katika maeneo hayo, sambamba na kukagua hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa ukaguzi, Mha. Besta ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuboresha mtandao wa barabara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Ukaguzi huo ni sehemu ya maandalizi ya hafla ya utiaji saini ya mikataba ya ujenzi wa barabara ya Mlowo–Kamsamba, inayounganisha mikoa ya Songwe, Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma; pamoja na barabara ya Mbalizi–Mkwajuni–Makongorosi, inayounganisha mikoa ya Songwe, Mbeya, Singida na Tabora. 

Aidha, Mtendaji Mkuu huyo ameongozana na timu ya wataalamu kutoka Makao Makuu ya TANROADS, chini ya uongozi wa Mha. Frank Mwakisonga, ambapo ametoa maelekezo ya kuhakikisha kazi za usanifu na maandalizi ya ujenzi zinakamilika kwa haraka na kwa viwango vinavyokubalika.

“Tunahitaji kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati, ili wananchi waanze kunufaika na miundombinu bora itakayorahisisha usafiri, kukuza biashara na kufungua fursa za maendeleo,” alisema Mha. Besta.

Miradi hii mikubwa ya barabara inatarajiwa kuimarisha mawasiliano kati ya mikoa na kusaidia jitihada za Serikali za kuunganisha maeneo yote ya nchi kwa mtandao thabiti wa barabara za lami.