News

NI HISTORIA RAIS SAMIA AFUNGUA RASMI DARAJA LA J.P. MAGUFULI

NI HISTORIA RAIS SAMIA AFUNGUA RASMI DARAJA LA J.P. MAGUFULI

Mwanza

19 Juni, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelifungua rasmi daraja la J.P. Magufuli lenye urefu wa kilomita 3 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 linalounganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema Mkoani mwanza.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo ni utekelezaji wa ndoto ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

"Miongoni mwa vitu nilivyoahidi ni kuendeleza miradi iliyoanzishwa na watangulizi wangu" amesisitiza Rais Dkt. Samia. 

Rais Samia ameeleza kuwa kukamilika kwa daraja hilo lililoko kwenye barabara kuu ya Usagara-Sengerema-Geita (km 90) litachochea uchumi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuunganisha Tanzania na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda. 

Ameongeza kuwa sasa wananchi watatumia dakika nne (4) kuvuka kupitia daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharamiwa na fedha za ndani kiasi cha  Bilioni 718 kukamilisha daraja hilo.

“Tanzania sasa inauwezo wa kupanga na kutekeleza miradi yake na asilimia 92 ya wajenzi ni Watanzania", amesema Rais Dkt. Samia.

Rais Samia amewataka wananchi kulitumia vizuri daraja hilo ili kuongeza tija na kuimarisha biashara za kikanda.

Aidha, Rais Samia amevitaka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na TANROADS kulilinda daraja la J.P. Magufuli,  ambalo ni la kimkakati na kulifanyia ukaguzi wa mara kwa mara ili lidumu kwa muda mrefu.

Vilevile, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kusimamia vizuri ujenzi wa daraja hilo kwa viwango vya ubora.

Naye, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kukamilika kwa daraja hilo ni furaha na fursa za uchumi kwa Watanzania wote.

"Hongera Mhe. Rais kwa bidii yako ya kutafuta fedha kukamilisha miradi ya miundombinu na huduma za jamii, hakika umefanya kazi kubwa", amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa miongozo na maelekezo yake yaliyowezesha kukamilika kwa daraja la J.P. Magufuli kwa wakati.

"Dkt. Samia alilikuta daraja liko asilimia 25 na fedha zilizolipwa shilingi Bilioni 152 lakini katika kipindi cha miaka minne amekamilisha ujenzi wote na kulipa fedha zote zilizobakia kwa Makandarasi na Wahandisi Washauri kwa wakati”, amesema.

Waziri Ulega amesema daraja hilo ni kielelezo cha nchi kufanya uamuzi, kusimamia miradi na kukuza uchumi wa watu wake.

Katika kuhakikisha msongamano wa magari unapungua jijini Mwanza  Waziri Ulega ameeleza kuwa Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa barabara njia nne kati ya jiji la Mwanza Mjini hadi Usagara (km 22).

Ameendelea kueleza kuwa Wizara itahakikisha vivuko vitatu vilivyokuwa vikitoa huduma kati ya Kigongo na Busisi vinahamishiwa katika maeneo mengine ya Ziwa Victoria kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma.

Daraja la J.P. Magufuli lenye urefu wa Km 3 ni daraja la saba (7) kwa urefu Barani Afrika na la sita (6) kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.