News

“RAIS WEWE NI MCHUNGAJI MWEMA UKIAHIDI UNATEKELEZA”- ULEGA

“RAIS WEWE NI MCHUNGAJI MWEMA UKIAHIDI UNATEKELEZA”- ULEGA

Mwanza

19 Juni, 2025

Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Hamis Ulega amemtaja Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Kiongozi mwenye hofu ya Mungu na mwenye kuahidi na kutekeleza yote anayowaahidi Watanzania, akimshukuru kwa maelekezo na msukumo wake katika miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali na kuifungamanisha na uchumi.

Mhe. Ulega amebainisha hayo leo Jumatano Juni 19, 2025 Jijini Mwanza wakati wa ufunguzi wa daraja la J.P Magufuli, zamani daraja la Kigongo-Busisi, akimuelezea Rais Samia kama Mchungaji mwema na kusema kwamba kukamilika na kuzinduliwa kwa daraja hilo ni kielelezo cha uwezo katika kufanya maamuzi na maendeleo ya Taifa la Tanzania.

"Wakati unapokea kijiti cha kuongoza Taifa letu Mhe. Rais, miradi hii ya kimkakati likiwemo daraja hili lilikuwa asilimia 25 tu na hapo tulikuwa tumelipa siyo zaidi ya Shilingi Bilioni 152. 

Daraja hili ukiweka na kodi ya ongezeko la thamani, thamani yake ni Bilioni 718, hivyo basi maana yake Rais Samia umelipa fedha za Kitanzania zaidi ya Bilioni 450 na ndiyo maana tunasema mama umeweza." Amesema.

Ulega amebainisha kuwa dhamira ya Rais Samia ni kuifunga Kanda ya Ziwa kiuchumi, akisema kujengwa kwa daraja hilo ni kiungo muhimu cha Stesheni kubwa ya mizigo ya reli ya SGR kueleka mikoa mbalimbali nchini na nchi za Afrika ikiwemo Uganda na Sudan Kusini.

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa ndani ya daraja hilo, ili kufanya shughuli za kijamii ikiwemo upigaji wa picha kurekodi matukio mbalimbali ikiwemo nyimbo za dini na kadhalika, mhusika atatakiwa kuomba kibali mapema kutoka kwa Wizara hiyo kupitia kwa Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza.

Ulega ametangaza habari njema pia za utanuzi wa barabara ya Mwanza Mjini - Usagara kuwa ya njia nne ili kukabiliana na msongamano unaoshuhudiwa sasa pamoja na ujenzi wa barabara ya Sengerema - Nyehunge, ambapo tayari mikataba imesainiwa na Mkandarasa ataanza kazi ya ujenzi hivi karibuni.