MTENDAJI MKUU TANROADS AKAGUA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA SHINYANGA, APONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI
Shinyanga
16 Juni, 2025
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta tarehe 16 Juni, 2025 amefanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga na kuagiza Mkandarasi anaetekeleza ujenzi huo kampuni ya CHICO, kuhakikisha anakamilisha kazi za kufunga taa za kuongozea ndege pamoja na kumalizia jengo la abiria kwa wakati.
Aidha, Mha. Besta amesema kwa sasa maendelea ya mradi kwa ujumla yamefikia aslilimia 82 huku sehemu ya kutua na kuruka ndege vikiwa vimekamilika kwa asilimia 100 na ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 72.
Amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi CHICO chini ya usimamizi wa Mhandisi Mshauri (SMEC International) pamoja na TANROADS na kusisitiza kuwa Mkandarasi aendelee kusimamiwa vyema ili kazi zilizobaki zikamilike kwa wakati.
Kazi zinazoendelea kwa sasa ni uwekaji wa miundombinu ya taa za kuongozea ndege (AGL system) na umaliziaji wa jengo la abiria (Terminal Building).
Kiwanja hiki kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120,000 kwa mwaka na kinatarajia kukamilika ifikapo Septemba 10, 2025.
Mha. Besta ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha inaboresha Sekta ya Usafiri wa Anga ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa taifa.