MTENDAJI MKUU WA TANROADS ATOA TAARIFA KWA RAIS SAMIA YA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA MSALATO
Dodoma
14 Juni, 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Jumamosi Juni 14, 2025 amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, ambapo amepokea taarifa fupi ya mradi kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta.
Katika taarifa hiyo, Mhandisi Besta ameeleza kuwa mradi huo mkubwa umegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inahusu ujenzi wa maeneo ya matembeleo ya ndege (movement areas) ikiwemo barabara ya kuruka na kutua ndege (runway), njia za maungio (taxiways) pamoja na maeneo ya maegesho ya ndege (apron).
"Ujenzi wa sehemu hii unatekelezwa na kampuni ya Sinohydro kwa gharama ya shilingi bilioni 165, na hadi sasa umefikia asilimia 89.9 ya utekelezaji." alisema Mhandisi Besta.
Ameendelea kw kusema kuwa, sehemu ya pili ya mradi inahusisha ujenzi wa majengo mbalimbali ambayo ni pamoja na jengo la abiria, jengo la zimamoto, jengo la hali ya hewa, jengo la kuongozea ndege pamoja na kituo cha kuzalisha nishati ya umeme (power station).
Ujenzi wa sehemu hii umefikia asilimia 55. Mhandisi Besta ameeleza kuwa uwanja huo umesanifiwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) ukiwa na code 4E, ambayo ni sifa ya uwanja wa ndege unaoweza kupokea ndege kubwa za umbali mrefu kama Boeing 777, Boeing 747, na hata Airbus A380 – ndege kubwa zaidi ya abiria duniani.
“Uwanja wa Msalato ni miongoni mwa viwanja vikubwa kabisa vya ndege katika ukanda huu" alisisitiza Mradi huu ni alama ya mafanikio na sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuijenga Dodoma kama mji Mkuu wa kisasa unaoendana na hadhi ya Taifa letu na ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya kuimarisha miundombinu ya usafara wa anga nchini na kufungua milango ya maendeleo kwa jiji la Dodoma, wananchi na Taifa kwa ujumla.