News

WAJUMBE KUTOKA MALAWI WATEMBELEA MRADI WA BRT AWAMU YA TATU "TUMEKUJA KUJIFUNZA KUTOKA TANROADS NAMNA YA KUTEKELEZA MIRADI MIKUBWA"

Ujumbe kutoka serikali ya Malawi ukiongozwa na mkurugenzi wa huduma za utawala kutoka Mamlaka ya barabara Malawi (Roads Authority of Malawi), Bw. Robson Piringu leo Alhamis Juni 12,2025 umetembelea mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya tatu jijini Dar es salaam kwa lengo la kujifunza kuhusu utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Rottoson Kabalika, msaidizi wa Meneja mradi wa BRT-3 kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), amesema kuwa mradi huo unaanzia Posta ya zamani na kupita katika barabara za Azikiwe, Maktaba, Bibititi, Nkuruma na nyerere hadi kufikia Gongo la mboto umbali wa takribani kilomita 18.

Ameeleza kuwa mradi umebuniwa kwa kuzingatia matumizi ya watembea kwa miguu na vyombo vyote vya usafiri, ambapo njia za mabasi zinajengwa kwa zege lenye uimara wa kudumu hadi miaka 30, wakati njia za magari mengine zinajengwa kwa lami na za waenda kwa miguu kwa kutumia paving blocks.

“Tumewatembeza wageni hadi Gongo la mboto na kuwaonesha maneo maaalum ya mradi ikiwemo vituo vya mabasi vinavyojengwa katikati ya barabara, wamevutiwa sana na wametupongeza kwa hatua iliyofikiwa ambapo mradi umefikia asilimia 90% na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30,2025” alisema mhandisi Kabalika.

Ameongeza kwa kusema kuwa baada ya kukamilika, mradi utakabidhiwa kwa Wakala ya Mabasi yaendayo Haraka Dar es salaam (DART) kwa ajili ya uendeshaji wa huduma za usafiri wa abiria.

Kwa upande wake, Bw. Piringu kutoka Malawi amesema lengo la ziara yao ni kujifunza kutoka TANROADS kuhusu mbinu bora za usanifu, utekelezaji na usimamizi wa miradi mikubwa ya barabara, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wao wa maendeleo wa miaka mitano unaohusu sekta ya miundombinu.

“Tulishauriana na wadau wetu wa ndani ikiwemo vitengo vya rasilimali watu na wataalamu mbalimbali na kuona kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa miradi ya barabara. Tumefurahia kujifunza kutoka TANROADS na ushirikiano mzuri uliopo kati ya taasisi hiyo, wakandarasi na washauri wa mradi” alisema Bw. Piringu.

Naye Mhandisi Hendrush Nyange, ambaye ni Mkandarasi Mshauri wa mradi huo, amesema kuwa asilimia kubwa ya vifaa vya ujenzi vimetolewa ndani ya nchi kama mawe, kokoto, mchanga na nondo, isipokuwa saruji na lami ambavyo vimeagizwa kutoka nje.

“Mradi umeajiri Zaidi ya watu 1000 na kazi kubwa imefanyika licha ya changamoto zilizojitokeza, ikiwemo kupitisha barabara katika maeneo nyeti kama uwanja wa ndege, vituo vya majeshi na polisi pamoja na miundombinu ya chini ya aridhi kama maji,umeme na mawasiliano”alisema mhandisi Nyange.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya mradi yametokana na ushirikiano thabiti kati ya TANROADS, Mkandarasi na Mkandarasi mshauri.