News

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA, YASAINI MIKATABA YA BIL. 55/- NA WAKANDARASI WANAWAKE

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA, YASAINI MIKATABA YA BIL. 55/- NA WAKANDARASI WANAWAKE

Dar es Salaam

10 Juni, 2025

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) tarehe 10 Juni, 2025 imeweka historia kwa kusaini mikataba minne ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, mikataba iliyolengwa mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wakandarasi wanawake nchini. 

Hafla hiyo ya kihistoria imeongozwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, huku thamani ya mikataba hiyo ikifikia jumla ya shilingi Bilioni 55.

Mha. Besta amesema, miradi hiyo inalenga kuboresha barabara ya Ruanda–Nyimbili – Hasamba – Humba yenye urefu wa kilomita 79.8, ambapo kila mkataba unahusu ujenzi wa kilomita tano kwa kiwango cha lami.

Amesema kazi hiyo imekabidhiwa kwa makampuni manne tofauti yaliyoundwa kwa ubia wa wanawake (JV Groups), yakijumuisha jumla ya kampuni 12 zinazomilikiwa na kuendeshwa na wanawake wa Kitanzania.

"Miradi hii si ya matengenezo bali ya kuinua hadhi ya barabara kutoka changarawe hadi kiwango cha lami, tunashukuru kwa msukumo mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alituagiza kuhakikisha mikataba hii inasainiwa na kusimamiwa kikamilifu ili ijengwe kwa ubora wa hali ya juu," alisema Mha. Besta.

Rais wa Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania, Mha. Judith Odunga, ameishukuru serikali kwa kuweka kihistoria hii isiyosahaulika kwa wanawake nchini.

"Ni mwaka 2020 tulipoomba kwa Rais Dkt. Samia kusaidia wakandarasi wanawake, leo miaka mitano baadaye, tumesaini mikataba mikubwa ya kihistoria, tunamshukuru sana mama yetu Rais kwa kutimiza ahadi yake, pia ninaishukuru Wizara ya Ujenzi, Bodi ya Wakandarasi (CRB), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na TANROADS kwa ujumla kwa ushirikiano wao kwetu," alisema Mha. Odunga

Mha. Odunga amefafanua kuwa kila mkataba mmoja unahusisha kampuni tatu, hivyo jumla ya kampuni 12 zitanufaika moja kwa moja na ajira kwa vijana wa maeneo husika zitapatikana kupitia utekelezaji wa miradi hiyo.

TANROADS imeahidi kushirikiana kwa karibu na wakandarasi hao wanawake ili kuwajengea uwezo na kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vya juu, ikiwa ni utekelezaji wa azma ya serikali ya kuwainua wakandarasi wazawa na kuleta usawa wa kijinsia katika sekta ya ujenzi.

Miradi hiyo ni ya aina yake na ya kwanza kutekelezwa kwa mkakati wa moja kwa moja wa kuwawezesha wakandarasi wanawake  kushiriki katika uchumi wa ujenzi wa miundombinu nchini.