BILIONI 24 KUJENGA BARABARA YA WASO - LOLIONDO
Arusha
09 Juni, 2025
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetia saini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Waso hadi Loliondo yenye urefu wa kilomita 10, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha kwa gharama ya Sh 24 Bilioni.Hafla hiyo imefanyika tarehe 09 Juni, 2025 na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Makonda amesema mradi huo ni miongoni mwa hatua madhubuti zinazochukuliwa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya barabara na kufungua fursa za maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.Amesema ujenzi wa barabara hiyo utaongeza mzunguko wa kiuchumi katika maeneo ya Loliondo, kuboresha huduma za kijamii na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu.
Mkandarasi China, Wu Yi Ltd amepewa jukumu la kutekeleza mradi huo na ametakiwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha barabara inakamilika ndani ya miezi 12 kama ilivyopangwa.