KASEKENYA ATAKA UJENZI WA BARABARA YA ISONGOLE -ISOKO KM 52 UENDE KWA KASI
Songwe
08 Juni, 2025
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameelekeza Mkandarasi anaejenga barabara ya Isongole-Isoko Km 52 kumsimamiwa kikamilifu, ili ikamilike kwa wakati.
Kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea ukuaji wa uchumi kwa wakazi wa Ileje na kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi.
Mha. Kasekenya amelekeza hayo Juni 8, 2025 kwa Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Songwe, wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo na kumtaka mkandarasi kutoa fursa nyingi za ajira kwa vijana na wanawake wa eneo hilo la mradi.
"Msimamieni Mkandarasi vizuri, tunatamani anavyoanza kwa kasi asimamiwe kwa kasi hiyo hiyo, Wananchi wanataka waone barabara inaanza kujengwa", amesisitiza Naibu Waziri Mha. Kasekenya.
Aidha, amekagua na kujionea ujenzi wa daraja la dharura lililopo Kata ya Sange Kijiji cha Sange.
Mha. Kasekenya amesema Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali na fedha za ujenzi wa barabara hiyo, hivyo hakuna sababu yoyote ya kutokufanya kazi kwa kasi.
Naibu Waziri Mha. Kasekenya yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua ujenzi wa miundombinu mkoani Songwe.