News

TANZANIA NA KOREA KUENDELEZA USHIRIKIANO SEKTA YA MIUNDOMBINU

TANZANIA NA KOREA KUENDELEZA USHIRIKIANO SEKTA YA MIUNDOMBINU

 

Dodoma

27/05/2025

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amekutana na kufanya mzungumzo na Makamu wa Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Hyun Hwan Jin pamoja na ujumbe wake leo, tarehe 27 Mei, 2025 katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

 

Katika kikao hicho Serikali ya Tanzania imeishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufadhili wa ujenzi wa Daraja la Tanzanite, jijini Dar es Salaam lenye urefu wa kilometa 1.03 na barabara unganishi Kilometa 5.2 ambalo limekamilika na linatumika.

 

Aidha, Naibu Waziri Mha. Kasekenya amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Taasisi za Korea za K-FINCO pamoja na KIND na Taasisi za Wakala wa majengo Tanzania (TBA) na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, ambao unajikita kwenye ufadhili wa miradi ya ujenzi wa miundombinu na miradi ya ubia kati ya Sekta Binafsi na Umma (PPP).

 

Kwa upande wake, Makamu wa Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Hyun Hwan Jin ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wanaowapa na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo na kuona namna makampuni ya Ujenzi ya Korea Kusini yanavyoweza kushiriki katika miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari na uendelezaji wa miji na majiji nchini.  

 

Kikao hicho kimehudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake ikiwemo TBA, TANROADS na TEMESA.